Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 26, 2024 Local time: 09:37

Hayati Mwinyi akumbukwa kwa kuwajibika, kuongoza mpito kuelekea demokrasia Tanzania


Marehemu rais wa zamani wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi
Marehemu rais wa zamani wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi

Rais mstaafu wa Tanzania, Mzee Ali Hassan Mwinyi, alifariki dunia Alhamisi katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu ya saratani ya mapafu.

Baadhi ya Watanzania, wakiwemo wanasiasa wanasema Rais huyo wa awamu ya pili atakumbukwa zaidi kama kiongozi shupavu aliyechukua usukani wakati taifa hilo likitoka kwenye vita vya Kagera na kufanikiwa kuimarisha uchumi wa nchi hiyo. Mwandishi wetu wa Dar es Salaam Amri Ramadhani anayo ripoti kamili.

Mwinyi alikuwa Rais wa pili wa Tanzania alieongoza kwa kipindi cha miaka kumi kuanzia mwaka 1985 hadi 1995 huku akiwa ni rais wa kwanza kuchaguliwa kwa njia ya kidemokrasia baada ya utawala wa chama kimoja.

Dkt Wilbroad Peter Slaa moja ya wanasiasa wakongwe nchini Tanzania amesema Rais huyo atakumbukwa zaidi kwa sera zake za kukaribisha uwekezaji ambazo zilileta unafuu wa maisha baada ya nchi kuwa imetoka kwenye vita vya kagera.

"Kwa hivyo Mzee Mwinyi alipokuja na sera yake ya kufungua madirisha na milango basi kila mkopo ukaingia vizuri na tukapata nafuu tofauti na kabla ya hapo, hiyo ni kuonyesha tu kwamba aliingia kipindi kigumu na akafanya kazi na Watanzania hawamsahau kwa hilo ndio maana wanamuita Mzee rukhsa," alisema Dr Slaa.

Rais Mwinyi alikuwa na mchango mkubwa katika kuleta mageuzi ya kiuchumi katika nchi ya Tanzania wakati wa uongozi wake alifanya mabadiliko makubwa katika kufungua milango kwa uwekezaji wa kigeni na kuanzisha sera za kuleta maendeleo ya kiuchumi ambayo yalipelekea kuongezeka kwa ufanisi katika sekta ya kilimo, viwanda na hudumu za kifedha.

Tundu Lissu ambae ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA amesema Mzee Mwinyi atakumbukwa zaidi kama Rais alieiingiza Tanzania katika mfumo wa vyama vingi na kuitoa katika mfumo wa chama kimoja.

"Mwinyi ndie rais aliyetuingiza katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, na ndiye alietuondoa katika mfumo wa kiimla wa chama kimoja. Tanzania ni nchi ya vyama vingi sasa hivi kwa sababu ya Mzee Mwinyi, ilitokea wakati wa urais wa Mzee Mwinyi," alisema Lisu.

Hata hivyo Naibu Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mussa Azan Zungu amesema Mzee Mwinyi atakumbukwa kama kiongozi aliekuwa muwajibikaji baada ya kuonyesha uwajibikaji pale alipojiuzulu nafasi ya Waziri wa mambo ya ndani baada ya wafungwa kufariki wakiwa mahabusu.

Zungu alisema: "Wafungwa walifariki jela nafikiri ilikuwa maeneo ya Shinyanga na akachukua jukumu la kisiasa kuona kwamba tukio lile lilimuaibisha yeye akiwa kama ni waziri mwenye dhamana ya mambo ya ndani akaamua kujiuzulu na kuomba mheshimiwa Rais Nyerere amkubalie ajiuzulu."

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akizungumza kupitia vyombo vya habari Alhamisi, alitangaza siku saba za maombolezo kufuatia kifo cha Rais huyo huku akitangaza maziko yatafanyika tarehe 02 ya mwezi Machi, Unguja visiwani Zanzibar.

-Imetayarishwa na Amri Ramadhani, Sauti ya Amerika, Dar es Salaam.

Forum

XS
SM
MD
LG