Akizungumza wakati akitoa salamu za pole kwa familia na wananchi wa Tanzania Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amesema njia nzuri ya kumuenzi hayati Edward Lowassa ni kufanya siasa za maridhiano na siasa za kujenga hoja, kuheshimiana, kustahamiliana bila kulumbana wala kutikisa misingi ya utaifa.
“Hapa tunapata somo kubwa sana la siasa za kujenga hoja, kuheshimiana, kustahamiliana na siasa za kuleta maendeleo huo ni ukomavu mkubwa wa kisiasa na ni njia nzuri ya kuchukua kama tunataka kumuenzi Lowassa na vitendo vyake”
Hata hivyo Rais Samia ameongezea kusema kuwa Lowassa ni kiongozi alieacha funzo kuwa watu wanaweza kutofautiana katika mitazamo na sera bila kuvunja misingi ya Utaifa wao.
“alichotufundisha ni kwamba tunaweza tukatofautiana mitazamo, misimamo na sera bila kutukanana kulumbana wala kutikisa misingi ya Utaifa na mshikamano wetu na bado tukaelewana” ameongezea Rais Samia
Kwa upande wa Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani CHADEMA Freeman Mbowe wakati akimuelezea Hayati Edward Lowassa amemtaja kama kiongozi aliyetoa mchango mkubwa katika kuimarisha demokrasia nchini Tanzania na mgombea wa kwanza kutoka upinzani kuonyesha ushindani katika uchaguzi.
“mheshimiwa Lowassa nae ni muhanga wa mifumo yetu ya uchaguzi lakini huyu alikuwa ni mgombea wa Urais katika upinzani wa kwanza kupata kura zaidi ya million sita halikuwa jambo dogo ni kwasababu ya karama ya huyu mzee”
Mbowe ameongezea kuwa “Nina imani kuwa utendaji kazi kamili wa Mheshimiwa Lowassa haukuwahi kupatikana hivyo tuwape watu nafasi za uongozi katika misingi ya kweli na haki taifa letu likapate viongozi wema ambao watatupeleka mbele wote kwa umoja wetu”
Lowassa aliefariki tarehe 10 ya mwezi februari katika taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete jijini Dar es Salaam ameacha Mjane mmoja Regina Lowassa pamoja na watoto watano kati yao wakiume watatu na wakike wawili.
Imeandaliwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika.
Forum