Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 26, 2024 Local time: 22:22

Maelfu ya watu wapoteza makazi Msumbiji


Watu waliopoteza kamazi kutoka jimbo la Cabo Delgado wakitembea katika wilaya ya Nampula February 27, 2024. Picha na Alfredo ZUNIGA / AFP.
Watu waliopoteza kamazi kutoka jimbo la Cabo Delgado wakitembea katika wilaya ya Nampula February 27, 2024. Picha na Alfredo ZUNIGA / AFP.

Serikali ya Msumbiji imethibitisha kwamba maelfu ya watu wamekoseshwa makazi kutokana na mashambulizi ya wanamgambo kaskazini mwa nchi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Maputo, msemaji wa serikali ya Msumbiji Filimao Suaze alisema watu 67,321 wamekoseshwa makazi katika mkoa wa Cabo Delgado.

Amesema watu hao wanaotoka familia 14,270 wamewasili katika mkoa wa Nampula na maeneo mengine.

Hata hivyo, amesema serikali haijafikia hatua ya kuamini kwamba hali hiyo ni dharura kwa kitaifa kutokana na mashambulizi ya Cabo Delgado.

Chiure Mendes Luciano mkimbizi mwenye umri wa miaka 23 kutoka mkoa wa Cabo Delgado, amesema wameshambuliwa na kundi la wanaume waliokuwa wakijihami kwa mapanga na bunduki.

"Makundi ya wanaume waliwasili na kuanza kuchoma moto magari. Tulijawa na hofu na kukimbilia hapa tangu Februari tarehe 20. Tumekuwa hapa kwa muda wa wiki moja na hatuna chakula. Sote tuliokuja hapa tunataabika sana,” amesema Luciano

Naye Josefina Gabriele, mkimbizi mwenye umri wa miaka 40 kutoka Chiure, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa waliyakimbia makazi yake Februari 20 na hana chakula wala pa kulala.

Alisema "Milio ya risasi ilituamsha kutoka kwa usingizi. Walianza kutufukuza. Tuliona wakikata vichwa vya wanaumme kwa kutumia panga na tukakimbia. Ni magaidi.”

Kulingana na shirika la uhamiaji la umoja wa mataifa IOM, Mapigano mapya yalianza wiki mbili zilizopita kaskazini mwa Msumbiji.

Umoja wa mataifa unasema kwamba watu 71,681 wamekimbia mashambulizi katika wilaya za Macomia, Chiure, Mecufi, Mocimboa da Praia na Muidumbe kati ya Desemba 22 na Februari 25.

Kati ya Jumatano na Alhamisi, IOM limerekodi zaidi ya watu 30,000 ambao wamewasili katika mji wa Namapa, kusini mwa Cabo Delgado, kwa kutumia basi, boti au kwa miguu.

Wanaokimbia wanahitaji msaada mkubwa wa chakula, makao na huduma ya afya.

Mashambulizi yalianza Oktoba 2017 wakati wapiganaji wanaodai kuwa sehemu ya kundi la kigaidi la Islamaic state, waliposhambulia sehemu za pwani kaskazini mwa Cabo Delgado ambapo kuna utajiri mkubwa wa mafuta, karibu na Tanzania.

Tangu July 2021, maelfu ya wanajeshi kutoka Rwanda na SADC, wameshika doria sehemu hiyo kusaidia jeshi la Msumbiji na wamefanikiwa kudhibithi sehemu kubwa ya Cabo Delgado.

Wanajeshi wa SADC wanatarajiwa kuondoka Msumbiji katikati mwa mwezi July.

Forum

XS
SM
MD
LG