Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 20:42

Ruto na Abiy wakubaliana kuimarisha uhusiano kati ya nchi zao


Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed (kushoto) na Rais William Ruto wa Kenya wakati awkikagua gwaride la heshima Februari 28, 2024.
Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed (kushoto) na Rais William Ruto wa Kenya wakati awkikagua gwaride la heshima Februari 28, 2024.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na Rais William Ruto wa Kenya wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wa raia wa nchi zao, kuondoa vikwazo vya usafiri na kuwezesha kuongezeka kwa biashara kati ya nchi hizo mbili.

Waziri mkuu wa Ethiopia yuko nchini Kenya kwa ziara ya kiserikali, na amekutana na mwenyeji wake rais Ruto ambako wamejadili masuala ya kidiplomasia, usalama na ushirikiano wa kiuchumi na utalii.

Viongozi hao wawili, ambao hawakuzungumza na wandishi wa habari jijini Nairobi siku ya Jumatano, walikuwa pia na majadiliano kuhusu masuala ya mafuta, nishati na faida za utekelezaji wa mradi wa Bandari ya Lamu, maarufu kama LAPSSET .

Mradi huo unasemekana ndio mkubwa zaidi wa miundombinu katika ukanda wa Afrika Mashariki unaoziunganisha Kenya, Ethiopia na Sudan Kusini, wenye thamani ya shilingi bilioni 17.9.

Baada ya kuzuru kituo cha Suswa, jimbo la Kajiado kinachowezesha kutoa huduma ya umeme kwa Kenya, Ethiopia na Tanzania, Rais Ruto na kiongozi huyo ya Ethiopia, wamesema wanatafuta ushirikiano wa kuunganisha makampuni ya umeme ya nchi zao ili kuimarisha na kupanua usambazaji na upunguzaji wa gharama ya nishati.

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed akikagua gwaride la heshima kumkaribisha Nairobi, Kenya kabla ya mazungumzo na mwenyeji wake Rais William Ruto.
Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed akikagua gwaride la heshima kumkaribisha Nairobi, Kenya kabla ya mazungumzo na mwenyeji wake Rais William Ruto.

Viongozi hao wameeleza kuwa upanuzi wa usambazaji wa nishati safi wa kikanda utakuza biashara nzuri, pasmoja na kupunguza uchafuzi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Kupitia taarifa ya pamoja kwa vyombo vya habari, Ruto na Abiy wameeleza kuwa majadiliano yao yana haja ya kuharakisha uhusiano unaoadumu wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili jirani, suala ambalo Nasongo Muliro, mfuatiliaji wa masuala ya kidiplomasia katika Pembe ya Afrika, anaeleza unaweza kufaulishwa kutokana na utekelezaji wa mradi wa LAPSSET.

"Kuhusiana na hali ya usalama katika Pembe mwa Afrika, Rais Ruto na Waziri Mkuu Abiy wanaeleza kuwa kuna haja ya kudumisha amani na kuweka utulivu kwa ukuaji na uendelevu wa uchumi, na kueleza kuwa hapafai kuwapo na mabadiliko yasiyo ya kikatiba ya serikali na kuingiliwa kwa michakato ya kisiasa ya ndani ya nchi za Kiafrika na masilahi ya nje."

Muliro anaeleza kuwa ziara hii itatumika kutafuta suluhisho kwa mzozo kati ya Ethiopia na Somalia kuhusiana na mkataba wa ufukwe, na jimbo la Somalia lililojitenga la Somaliland.

Somaliland ilikuwa sehemju kamili ya Somalia karibu na Ghuba ya Aden, na ilijitangazia uhuru wake kutoka Mogadishu 1991, ingawa haijatambuliwa kama taifa na jumuia ya kimataifa.

Wakati huo huo Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, yuko pia Nairobi, kuhudhuria mkutano wa viongozi wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa UNEA.

Kupitia mitandao yao ya X, Abiy amesema majadiliano kati yake na Ruto yamelenga kuimarisha uhusiano uliopo lakini pia yameangazia maeneo muhimu ya ushirikiano wa siku zijazo. Huku Ruto akieleza kuwa uhusiano wa muda mrefu kati ya Kenya na Ethiopia ndio msingi wa ustawi wa pamoja na utulivu wa kikanda.

Hii ripoti imetayarishwa na Kennedy wandera mwandishi wa Nairobi

Forum

XS
SM
MD
LG