Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 23:15

Rais wa zamani wa Tanzania Benjamin Mkapa, 81, afariki


Aliyekuwa rais wa Tanzania, Benjamin Mkapa
Aliyekuwa rais wa Tanzania, Benjamin Mkapa

Aliyekuwa rais wa Tanzania Benjamin Mkapa amefariki. Mkapa aliaga dunia usiku wa kuamkia Ijumaa katika hospitali moja mjini Dar es Salaam.

Rais John Magufuli alitangaza kifo cha kiongozi huyo wa zamani, ambaye alikuwa rais wa awamu ya tatu, kupitia taarifa fupi iliyorushwa moja kwa moja kwa njia ya televisheni kutoka Ikulu mwendo wa saa sita na dakika ishirini na tano saa za Afrika Mashariki.

"Kwa masikitiko makubwa tumepata msiba mkubwa. Mzee wetu, rais wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa amefariki akiwa hospitalini mjini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa," alisema Rais Magufuli.

"Tuendelee kumuombea Mzee Mkapa ambaye ametangulia mbele ya haki," aliongeza, bila kutoa maelezo zaidi.

Kabla ya kuwa rais, Mkapa alikuwa miongoni mwa wanadiplomasia waandamizi wa Tanzania akishika nafasi kama waziri wa mambo ya nje na balozi wa Tanzania katika utawala wa rais wa kwanza, Mwalimu ulius Nyerere na rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi.

Wakati wa uongozi wake Mkapa alisifiwa kwa kuweka taratibu na kanuni nyingi za shughuli za kiserikali na kuzifanya idara za serikali zifanye kazi kwa ufasaha zaidi.

Kimataifa Mkapa alikuwa miongoni mwa viongozi waliohusika sana kwenye juhudi za kiuchumi na kutatua migogoro barani Afrika na katika ushirikiano wa kiuchumi wa nchi za kusini-kusini.

Mara ya mwisho Mkapa alionekana hadharani wiki mbili zilizopita mjini Dodoma katika mkutano wa taifa wa chama tawala cha mapinduzi CCM kilichomteua Rais Magufuli kugombania awamu ya pili ya uongozi nchini katika uchaguzi wa Oktoba 28.

Risala za rambirambi zilianza kutolewa punde tu baada ya tangazo hilo la Rais Magufuli kuhusu kifo chake.

"Mzee Mkapa daima atakumbukwa kwa juhudi zake za upatanishi katika eneo la Afrika Mashaiki na Kati," alisema Profesa Patrick Nighula, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha South Carolina na mchambuzi wa masuala ya siasa, katika mahojiano na Sauri ya Amerika siku ya Alhamisi.

Mkapa, ambaye alikuwa rais wa Tanzania kuanzia mwaka wa 1995 hadi 2005, alizaliwa Novemba 12, 1938. Amemuacha mjane, Anna Mkapa, na watoto.

XS
SM
MD
LG