Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 26, 2024 Local time: 10:24

Tanzania: Wasomi waonyesha matumaini na ziara ya Rais wa Romania katika nyanja ya kilimo


Rais Samia Suluhu Hassan akimpokea Rais wa Romania Klaus Iohannis, Ikulu Dar es Salaam
Rais Samia Suluhu Hassan akimpokea Rais wa Romania Klaus Iohannis, Ikulu Dar es Salaam

Wasomi nchini Tanzania wanatarajia ushirikiano kati ya taifa hilo na taifa la Romania utaongeza na kukuza uzalishaji katika sekta ya kilimo iwapo makubaliano yaliyofikiwa baina ya mataifa hayo yatatekelezwa kikamilifu.

Hayo yamesemwa kufuatia Marais wa mataifa hayo mawili, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na mgeni wake Rais Klaus Iohannis kushuhudia utiaji saini wa hati za makubaliano katika maeneo ya kimkakati ikiwemo kilimo, mazingira na ushirikiano katika kukabiliana na majanga.

Akizungumza na Sauti ya Amerika mchambuzi wa mahusiano ya kimataifa kutoka chuo kikuu cha Dodoma, Justine Kajerero anasema Tanzania ina nafasi ya kunufaika na makubaliano hayo iwapo makubaliano yatatekelezwa vizuri kwa vile makubaliano ya ushirikiano huo yameanzia katika taaluma, vyuo na wataalamu.

“Nafasi ya Tanzania kunufaika ipo iwapo makubaliano yatatekelezwa vizuri, na uzuri tofauti ya wao na wengine ukiangalia kilimo wananchokiongelea wameanzia katika mahusiano ambayo yatahusisha taaluma, vyuo, na wataalamu kwasababu wengi wamekuwa wakija mara nyingi wanakwenda moja kwa moja kwenye mazao tofauti na taaluma ambayo ndio itasaidia kukuza kilimo” amesema Kajerero

Hati hizo mbili zilizosainiwa zinahusu kukuza ushirikiano wa kiuchumi Kisayansi na Kiufundi katika sekta ya kilimo na mazingira pamoja na utiaji saini kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Romania kwa ajili ya kushirikiana katika kukabiliana na maafa na misaada ya kimataifa ya kibinadamu.

Suala ambalo Dkt Eliaza Mkunaa, Mhadhiri mwandamizi kutoka chuo kikuu cha Mzumbe Morogoro anasema matarajio ya Watanzania ni kuona namna ambavyo wanaweza kunufaika na teknolojia pamoja na ujuzi kutoka Romania.

Amesema Mkuna “Tunategemea kuona namna ambavyo tunaweza kunufaika na teknolojia, ujuzi pamoja na mbinu mbalimbali za kuongeza tija kwenye kilimo kutoka Romania kwasababu ni nchi ambayo tumekuwa na mahusiano nayo kwa muda mrefu hivyo ni wakati muhimu sana ambao tunaweza kubadilishana uzoefu na kuongeza tija kwenye kilimo chetu.”

Dkt Mkuna ameongeza kusema kuwa kutokana na athari za mazingira zinazoendelea kujitokeza Duniani wanatarajia kuona tafiti mbalimbali zikifanyika na vyuo vilivyoingia makubaliano ili kukabiliana na changamoto zitokanazo na athari za mazingira.

“Tunajua kuwa dunia inapitia changamoto za mabadiliko ya tabia nchi hivyo tunategemea kuona tafiti mbalimbali zikifanyika na nchi hizi mbili kupitia taasisi zake mbalimbali ikiwemo vyuo vikuu, Chuo Kikuu cha Sokoine kikiwa miongoni mwa taasisi hizo na vyuo vingine vipate nafasi ya kuhusishwa katika tafiti hizo ili kuhakikisha tunaweza kuongeza tija ya uzalishaji pamoja na usalama wa chakula” amesema Mkuna

Naye Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na waandishi wa habari ameiomba Serikali ya Romania kuiunga mkono Tanzania katika mkutano wa Mabadiliko ya Tabia nchi wa COP28, 2023 utakaofanyika katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) katika ajenda yake ya nishati na nishati safi ya kupikia.

“Tumezungumzia ushiriki wetu kwenye COP28 ambao utafanyika pale Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) tumezungumza maeneo gani twende tukapeane nguvu katika mkutano ule lakini la muhimu zaidi tumewaomba wakatusaidie katika kutupa nguvu katika suala la Nishati na Nishati safi ya kupikia ili tusaidiwe kama inavyostahili” amesema Rais Samia

Rais wa Romania pia alikwenda Zanzibar ambako alikuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar Hussein Ali Mwinyi Rais kabla ya kuhitimisha ziara yake ya siku nne nchini Tanzania.

Amri Ramadhani Sauti ya Amerika Dar es Salaam

Forum

XS
SM
MD
LG