Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 09:13

Uchaguzi wa Tanzania 2020: Wapiga kura kuamua Jumatano


Ramani ya Tanzania
Ramani ya Tanzania

Magufuli anakabiliwa na ushindani kutoka kwa wagombea 15 akiwemo mpinzani mkuu Tundu Lissu mwenye umri wa miaka 52, anayegombea urais kwa tiketi ya chama cha upinzani – Chadema.

Wapiga kura nchini Tanzania kesho Jumatano wanapiga kura, katika uchaguzi ambao ni mtihani kwa rais wa sasa John Magufuli kutokana na utawala wake ambao umelezewa ni wa kimabavu, baada ya miaka mitano ya ukandamizaji kwa wapinzani na uhuru wa kujieleza.

Wapiga kura wa Tanzania bara na visiwani Zanzibar watapiga kura kumchagua rais na wabunge baada ya kampeni zilizoshuhudia idadi kubwa ya watu waliojitokeza kwenye mikutano ya kampeni ya vyama vyote vya siasa.

Magufuli anakabiliwa na ushindani kutoka kwa wagombea 15 akiwemo mpinzani mkuu Tundu Lissu mwenye umri wa miaka 52, anayegombea urais kwa tiketi ya chama cha upinzani – Chadema.

Lissu alirejea Tanzania mwezi Julai baada ya kuwa nje ya nchi kwa zaidi ya miaka mitatu, akipatiwa matibabu baada ya kunusurika kifo kwa kupigwa risasi 16, katika tukio lililotajwa kuwa jaribio la kumuua kwa sababu za kisiasa.

Kurejea kwa Lissu, kumeongeza nguvu kati ya wanasiasa wa upinzani.

Wanasiasa kadhaa wamekuwa wakikamatwa na kuripotiwa kushambuliwa, huku makundi ya kutetea demokrasia yakisema kwamba ni jaribio la utawala kukandamiza demokrasia.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, alitoa taarifa akiwa New York, akiwasihi “viongozi wa kisiasa Tanzania na wafuasi wao kushiriki katika zoezi hili kwa njia ya amani na kujizuia na ghasia.”

Ushirikiano wa vyama vya upinzani na siasa za Zanzibar

Kiongozi wa chama cha Upinzani cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, alimuidhinisha Tundu Lissu kuwa mgombea wa urais Tanzania bara, akisema kwamba “ana nafasi nzuri ya kumshinda rais Magufuli katika uchaguzi wa rais.”

Chama cha Chadema kinamuunga mkono mwanasiasa mkongwe wa chama cha ACT Wazalendo Seif Sharif Hamad, katika jaribio lake la sita kugombea urais visiwani Zanzibar.

Sharif Hamad, anashindana na mgombea wa chama tawala cha CCM, Hussein Ali Hassan Mwinyi.

Zanzibar ina historia ya kutokea ghasia za uchaguzi. Kampeni za Zanzibar kwa kiasi kikubwa zimekuwa za amani.

Visiwa vya Zanzibar vina wapiga kura 566,000 na kampeni zilimalizika jumapili, kila chama kikihitimisha kampeni kwa mikutano mikubwa.

Ushindani Tanzania bara

Wapiga kura milioni 29 wamesajiliwa Tanzania bara.

Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa moja asubuhi na kufungwa saa kumi alasiri saa za Afrika mashariki.

Hakuna ukusanyaji maoni uliofanywa kujua anayeongoza kwenye uchaguzi huo.

Kuna ripoti kwamba baadhi ya wagombea wa viti mbalimbali hasa wa upinzani, wamekuwa wakizuiliwa kufanya kampeni, balozi wa Marekani Donald Wright akieleza wasiwasi wake kwa matukio hayo.

“Nimefadhaika na ripoti ambazo nimeona na kuzisikia kwamba maafisa wa serikali na wa usalama wamekuwa wakivuruga mikutano ya kampeni ya baadhi ya wagombea,” amesema balozi wa Marekani Donald Wright katika ripoti ya maandishi, akiongezea kwamba “tunavyokaribia siku ya uchaguzi, visa vya kuvuruga mikutano ya wanasiasa wa upinzani vimekuwa ikiongezeka sana.”

Utawala wa kidikteta

Kwa miaka mingi, Tanzania imekuwa ikijulikana na majirani zake kama nchi thabithi na ya kidemokrasia. Lakini hali ya wasiwasi imeongezeka kwamba nchi hiyo imeanza kuingia katika utawala wa kidikteta, tangu kuchaguliwa kwa rais Magufuli mwaka 2015.

Magufuli, mwenye umri wa miaka 60 alianza kuchukua hatua zilizosifiwa na wananchi wa Tanzania, alizotaja kama kubana matumizi ya pesa za serikali kwa manufaa ya raia. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kupiga marufuku safari za nje ya nchi za wafanyakazi wa serikali wakiwemo mawaziri.

Alikuwa pia akifanya safari za kushutukiza katika ofisi za serikali, shuleni na hospitali kuhakikisha kwamba wafanyakazi wa serikali wanafanya kazi zao inavyostahili.

Alichukua hatua kali sana kupiga marufuku mikutano ya kisiasa na kuanza kubana wakosoaji wake.

Sheria kali dhidi ya vyombo vya habari zilipitishwa, waandishi wa habari wakaanza kukamatwa, sawa na wanaharakati na wanasiasa wa upinzani.

Mafanikio ya Magufuli

Magufuli anajivunia kuimarisha mfumo wa elimu bure kwa wote, kuunganisha umeme vijijini, ujenzi wa reli ya kisasa, barabara, bwawa la kuzalisha umeme na kufufua shirika la ndege la taifa.

"Nitawashangaza kwa kuanzisha miradi mingine mingi ya maendeleo iwapo nitashinda uchaguzi huu. Niliyofanya kwa miaka 5 ni kidogo sana ya yale ninayopanga kufanya,” alisema Magufuli katika mojawapo ya mikutano yake mikubwa ya kampeni.

Serikali ya Magufuli vile vile imepitisha sheria kadhaa zenye lengo la kuiletea faida serikali ya Tanzania kutoka kwa sekta yake ya madini na kutaka kampuni za kuchimba madini kutoka nchi za nje kuilipa Tanzania mamilioni ya dola kama ushuru.

Hata hivyo wachambuzi wamekosoa mtindo wa uongozi wa Magufuli, wakidai kwamba umewatisha wawekezaji.

Japo uchumi wa Tanzania umekuwa ukiimarika kabla ya kutokea janga la virusi vya Corona hadi kufikia asilimia 6, nafasi za ajira ni kidogo sana na mfumo wa ukusanyaji ushuru unaripotiwa kuathiri ukuaji wa sekta binafsi na kuweka mazingira magumu ya kufanya biashara nchini humo.

Shirika la kimataifa la fedha duniani IMF, linatarajia kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania kupungua kwa asilimia 1.9 mwaka huu.

Wasiwasi wa uchaguzi huru na haki

Kampeni zimefanyika katika mazingira ya kawaida licha ya kuwepo janga la Corona ulimwenguni. Tanzania ilisitisha kupima na kutoa takwimu za maambukizi ya virusi vya Corona mwezi April na rais Magufuli alitangaza kwamba virusi vya Corona vilishindwa nguvu nchini humo kutokana na nguvu za maombi.

Wanasiasa wa upinzani na wachambuzi hata hivyo wana wasiwasi na matokeo ya uchaguzi huo ambao unasimamiwa na tume ya uchaguzi inayoteuliwa na rais Magufuli.

Wafuatiliaji wa uchaguzi huo pia wameelezea wasiwasi wao kutokana na matukio ya kila mara, ya wanasiasa wa upinzani kushambuliwa katika kampeni na hata mikutano yao kutawanywa na maafisa wa polisi wanaowarushia gesi ya kutoa machozi, pamoja na mgombea wa upinzani Tundu Lissu kupigwa marufuku kufanya kampeni kwa muda wa siku 7 baada ya kudai kwamba kulikuwa na njama za kufanya udanganyifu katika hesabu ya kura.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG