Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 04:15

Mchango wa hayati Benjamin Mkapa kitaifa na kimataifa kama mwanadiplomasia


Hayati Benjamin Mkapa
Hayati Benjamin Mkapa

Marehemu Rais Benjamin William Mkapa aliyefariki usiku wa kuamkia tarehe 24 Julai, 2020 ni kiongozi ambaye anajulikana sana katika medani ya kisiasa na kidiplomasia kwa mchango wake mkubwa nchini Tanzania na nje ya taifa hilo.

Mkapa alishika wadhifa wa urais Novemba 23, mwaka 1995 baada ya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi nchini humo na kuliongoza taifa hilo kwa awamu mbili mpaka Desemba 21, mwaka 2005.

Atakumbukwa kwa harakati zake za kisiasa na pia kama mwanadiplomasia aliyebobea siyo tu kwa kushika wadhifa wa ubalozi na waziri wa mambo ya nje wa tanzania kwa muda mrefu lakini pia alikuwa mmoja wa viongozi ambao walikuwa mstari wa mbele katika kujihusisha na siasa za kieneo na kusimamia harakati za kuleta amani katika eneo hilo la Maziwa Makuu.

Tanzania

Akitangaza kifo cha Mkapa Ijumaa Rais John Magufuli alisema : “Kwa masikitiko makubwa tumepata msiba mkubwa, Mzee wetu Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu amefariki dunia, amefariki dunia katika hospitali Jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa, niwaombe Watanzania tulipokee hili, tumepata msiba mkubwa na tuendelee kumuombea mzee wetu Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa ambaye ametangulia mbele za haki, taarifa zingine zitaendelea kutolewa lakini Mzee Mkapa hatunaye tena,” Rais Magufuli alisema katika taarifa yake kwa Taifa.

Marehemu Mkapa ni rais pekee wa Tanzania ambaye kabla ya kuingia katika siasa alikuwa mwana habari aliyebobea. Mwaka 1966, Mkapa aliteuliwa kushika wadhifa wa mhariri wa gazeti la serikali la Tanzania Nationalist, ambapo mwaka 1972 alifanya kazi katika magazeti ya Daily News na Sunday News na mwaka 1974 aliteuliwa Katibu wa Habari wa Rais wa kwanza wa Tanzania Julius Kambarage Nyerere na kutokana na kazi yake hiyo mwaka 1976 alishiriki katika kuanzishwa rasmi kwa shirika la habari Tanzania – SHIHATA.

Mwanahabari mkongwe nchini Tanzania ambaye aliwahi kufanya kazi na Mkapa, Jenerali Ulimwengu ameiambia Sauti ya Amerika (VOA) Mkapa atakumbukwa kwa mengi. Aliwahi kutumikia wadhifa wake kama Waziri wa Mambo ya Nje na pia wa Habari na Utamaduni. Pia aliwahi kushika Wizara ya Sayansi na Teknolojia na Elimu ya Juu.

Wanasiasa wenzake wanamuelezea kuwa alikuwa si mtu ambaye anapenda kusema au kufanya jambo bila ya kuwa na uhakika. Mkapa alichukuwa madaraka ya urais baada ya Rais wa pili wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi kumaliza uongozi wake wa miaka kumi ambapo, alikuwa ameanzisha program za kulegeza uchumi, na Mkapa alipoingia madarakani program hiyo aliipa kipaumbele.

Burundi

Rais Mkapa hakujishughuisha kwenye siasa peke yake, alijihusisha katika harakati za upatanishi wa kieneo ili kuleta amani na usalama katika taifa la Burundi. Alikuwa mwenyekiti wa mkutano wa mazungumzo ya amani ya Burundi ambapo aliwaleta pamoja wawakilishi wa serikali ambayo ilikuwa chini ya uongozi wa marehemu rais Pierre Nkurunziza na upinzani ili kutafuta suluhisho kwa amani na usalama wa taifa hilo.

Aliteuliwa Julai mwaka 2015 baada ya kutokea machafuko nchini Burundi kufuatia marehemu rais Pierre Nkurunziza kuelezea azma yake ya kuwania muhula wa tatu madarakani. Utaratibu wa amani ulikumbwa na vikwazo na mivutano kati ya pande ambazo zilikuwa zinahusika katika mgogoro wa Burundi. Na mara kwa mara alielezea kusikitishwa kwake kuwa mazungumzo ya amani hayasongi mbele kwa vile upande mmoja katika mazungumzo hayo unakuwa haupo kwenye meza ya majadiliano ili kusukuma mbele juhudi za kupatikana kwa amani.

Wanasiasa wa Burundi na pia wengine katika eneo hilo watamkumbuka Mkapa kwa jitihada kubwa aliyoifanya kuona kuwa mafanikio yanapatikana.

Wanasema atakumbukwa katika eneo na kimataifa kwa juhudi zake kubwa za kuleta mafanikio katika taifa lake na majirani zake. Baada ya kuondoka madarakani alishika nyadhifa mbali mbali kimataifa - mwenyekiti wa South Centre, mwenyekiti mwenza wa Investment Facility for Africa – AWF, kamishna wa Umoja wa Mataifa kuhusu Kuwawezesha Kisheria Maskini na pia mwanachama wa baraza la Interaction.

Kenya

Mkapa atakumbukwa kwa mchango wake wa kufuatilia mjadala wa mabadiliko ya katiba nchini Kenya na kusema “sisi kama watanzania tunaona kuwa hili ni jambo jema kidemokrasia” na tunaweza kulitupia jicho.

Habari za kifo cha Mkapa zimewashitua Wakenya wameshtushwa na kifo cha Mkapa. Mmoja ya sifa zake Mkapa alikuwa mkosoaji mkali wa masuala mbali mbali lakini hakuwa akificha kutoa pongezi zake pale anapoona jambo jema limefanyika. Aliwapongeza watu wa Kenya kwa kufanikisha malengo makubwa ya ukuaji wa uchumi na kukumbatia mfumo kidemokrasia wa siasa. Na kubainisha hata mafanikio ya majirani yalikuwa ni kichochea kwa taifa lake.

Lakini hakuwa tu akijishughulisha na masuala ya Burundi na Kenya bali hata mataifa mengine katika eneo hilo la Maziwa Makuu.

Alikuwa mstari wa mbele kuzungumzia kuongezeka kwa mivutano kati ya Burundi na Rwanda na kusema kuwa kuna umuhimu mkubwa sana wa kuhakikisha kuwa nchi hizo jirani zinafanya mazungumzo ili kupata suluhu ya kudumu ili kuepuka mivutano zaidi.

Uhusiano kati ya Burundi na Rwanda ulidorora baada ya Bujumbura kuishutumu Kigali kupeleka majasusi kwenye mipaka yake, dai ambalo Rwanda ililikanusha vikali sana. Lakini shutuma hizo tayari zilijenga uhusiano wenye doa kati ya mataifa hayo mawili licha ya juhudi za Mkapa.

Leo hii wanyarwanda wana mengi ya kusema na kumkumbuka marehemu Mkapa ambaye alikuwa ni kioo kikubwa katika eneo hilo la Afrika Mashariki.

XS
SM
MD
LG