Mkuu wa polisi wa jiji hilo, James Cervera amesema mshambuliaji aliyetumia silaha ya moto“mara moja na bila ya kuchagua aliwapiga risasi wahanga wote wa shambulizi hilo” alipoingia katika jengo la manispaa baada ya saa kumi jioni Ijumaa.
Amesema wengine sita walikuwa wamejeruhiwa katika shambulizi hilo la bunduki.
Cervera amemuelezea mtu huyo aliyekuwa na bunduki ni mfanyakazi wa muda mrefu wa huduma za umma za jiji hilo aliyekuwa na chuki, lakini hakueleza zaidi nini kilipelekea kufanya shambulizi hilo.
Cervera amesema wanamjua mshukiwa huyo ni nani lakini bado wakati haujafika wa kutaja jina lake.
“Tutamtaja jina lake mara moja tu,” amesema, “na baada ya hapo ataendelea kutajwa kama “mshukiwa huyo” kwa sababu lengo letu sasa ni kuwapa heshima na taadhima wahanga katika tukio hili na familia zao.”
Walioshuhudia tukio hilo wanasema shambulizi hilo la bunduki lilitokea katika Jengo la Pili ya ofisi za manispaa zaVirginia Beach, ambako idara ya kazi za umma, huduma za umma na mipango ndio iliko.
Cervera amesema afisa polisi mmoja ni kati ya wale waliojeruhiwa lakini amenusurika. Mkuu huyo wa polisi amesema majibishano ya risasi na maafisa wa polisi yalisaidia kumzuia mtuhumiwa huyo kuuwa watu wengi zaidi.
Amesema uchunguzi juu ya shambulizi hilo ndiyo kwanza umeanza, lakini amesema polisi wanaamini mshukiwa huyo alikuwa peke yake katika kutekeleza uhalifu huo.
Mtu huyo alikuwa na bastola aina ya 45-caliber iliyokuwa na kifaa cha “kuzuia sauti” na risasi za ziada katika magazini zaidi ya moja ambayo aliweza kuzipandisha katika silaha hiyo kwa mfululizo katika shambulizi hilo.
“Ukweli wa kuwa mshukiwa huyo aliweza kudhibitiwa mara moja, ukweli wa kuwa mshukiwa huyo ameuawa, inamaanisha kuwa raia wanaweza kuwa na amani usiku wa leo,” amesema.
“Hii ni siku ya huzuni kubwa katika historia ya eneo la Virginia Beach,” amesema Meya Bobby Dyer katika mahojiano na waandishi wa habari ambaye alikuwa pamoja na mkuu wa polisi. “Wale walioathiriwa na shambulizi hili ni rafiki zetu, wafanyakazi wenzetu, majirani na watu warika letu.
White House imesema Rais wa Marekani Donald Trump alikuwa tayari amepewa taarifa fupi juu ya tukio hili na anaendelea kufuatilia suala hili.
Gavana wa Virginia, Ralph Northam, amesafiri kuelekea Pwani ya Virginia na ametangaza atatoa msaada kamili kutoka katika ofisi ya jimbo lake.
“Hili jambo halielezeki, uvunjifu wa amani wa kijinga kabisa,” amesema katika tamko lake.
Seneta wa Virginia Mark Warner amesema katika tamko lake “ Mimi nilishtushwa na kile kilichotokea leo katika eneo la Virginia Beach.”