Baada ya mshukiwa huyo kuondoka mahakamani, jaji alisema kuwa wakati kuna shtaka moja la mauaji lililoletwa hivi sasa, itakuwa ni sawa kufikiria kuwa kutakuwa na tuhuma nyingine dhidi yake.
Washukiwa wawili washiriki katika mauaji hayo pia wako chini ya udhibiti wa polisi. Polisi wanajaribu kufahamu kwa kiasi gani, iwapo wawili hao pia walihusika na shambulizi hilo.
Tarrant arejeshwa rumande
Tarrant mwenye umri wa miaka 28 ambaye ni raia wa Australia, akiwa amefungwa pingu alisimama kimya mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Christchurch kabla ya kurejeshwa rumande bila ya kusema chochote.
Kesi hiyo itasikilizwa tena April 5 na polisi wameeleza kuwa huenda mashtaka dhidi yake yakaongezeka.
Shambulizi la kigaidi
Shambulizi hilo ambalo limetajwa na serikali ya New Zealand kuwa nila kigaidi ni baya kabisa kuliko shambulizi lolote katika historia ya nchi hiyo.
Tarrant ni mwenye itikadi binafsi ya ubaguzi wa rangi kuwa wazungu ni bora kuliko watu wengine wote, alikuwa amefikishwa mahakamani na walinzi wawili wenye silaha za moto huko Christchurch ambapo jaji alisoma moja ya mashtaka ya mauaji yanayomkabili.
Dhamira ya muuaji
Katika mkutano na waandishi wa habari, Waziri Mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern amesema shambulizi la Tarrant dhidi ya Waislam hao msikitini lilisita tu kwa sababu mtuhumiwa huyo alidhibitiwa. “ Ilikuwa ni nia yake kuendelea na mauaji hayo,” amesema waziri mkuu.
Ameyaita mauaji hayo ni “kitendo cha uvunjifu wa amani kitendo kisichokuwa cha kawaida,” na kuahidi kuwa “sheria zetu za kumiliki silaha zitabadilishwa.” Alisema mshambuliaji huyo alikuwa na bunduki tano, mbili kati ya hizo zilikuwa ni silaha zenye kutoa risasi mfululizo. Silaha zote hizo zilikuwa zimenunuliwa kihalali.
Hatma ya washiriki wa mauaji hayo
Amesema kuwa wote mshambuliaji na washiriki wake katika tukio hilo la mauaji hawakuwa katika orodha ya watu wanaofuatiliwa na vyombo vya usalama vya New Zealand au Australia.
Waziri Mkuu wa Australia Scott Morrison ameeleza kuwa mshukiwa huyo ni “gaidi mwenye itikadi kali wa mrengo wa kulia.”
Tukio katika ibada ya Ijumaa
Shambulizi hilo limetokea wakati wa sala ya Ijumaa wakati misikiti yote miwili ilipokuwa imejaa mamia ya waumini wa Kiislam.
Maafisa wanasema kuwa watu 41 waliuawa katika Msikiti wa Al Noor, na wengine saba katika Msikiti wa Linwood, ambayo iko umbali wa dakika kumi baina yao. Watoto ni kati ya watu 48 wanaoendelea kutibiwa kutokana na majeraha ya risasi.