Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 09:49

Shambulizi la Msikitini New Zealand : Maombi maalum ya siku ya Ijumaa yafanyika, Imaam ampongeza Waziri Mkuu Ardern


Waombolezaji wikionyesha umoja baada ya ibada ya maziko iliyofanyika katika uwanja wa makaburi ya Memorial Park, Christchurch, New Zealand, Ijumaa, Machi 22, 2019.
Waombolezaji wikionyesha umoja baada ya ibada ya maziko iliyofanyika katika uwanja wa makaburi ya Memorial Park, Christchurch, New Zealand, Ijumaa, Machi 22, 2019.

Maelfu ya watu wamekusanyika siku ya Ijumaa kwa ajili ya maombi katika makaburi ya New Zealand ambapo wahanga 26 kati ya 50 wa mauaji ya pamoja ya shambulizi la bunduki ndani ya misikiti ya Ijumaa wiki iliyopita wamezikwa. Muhanga mdogo kuliko wote aliyezikwa alikuwa na umri wa miaka mitatu.

Mapema, katika ibada iliyofanyika nje karibu na msikiti ambako shambulizi hilo la mauaji lilitokea mjini Christchurch, Imam Gamil Fouda aliwahutubia maelfu ya watu waliohudhuria ibada hiyo, akiwaambia kuwa “Tumehuzunishwa lakini hatusambaratishwa.”

Aliuambia umati huo “chuki itaondolewa na upendo utarejeshwa kwetu.”

Imam huyo aliwashukuru “majirani ambao walifunguwa milango yao kutuokoa wakati tunamkimbia muuaji” na wale wote waliosimamisha gari yao kutusaidia.”

Fouda pia ametambua kitendo cha Waziri Mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern kwa “ kuziunganisha familia zetu pamoja na kutupa heshima ya kuvaa scafu ya kawaida kichwani. Amesema uongozi wa waziri mkuu ni somo kwa ulimwengu wote.”

Wanawake nchini kote New Zealand wanavaa skafu kichwani Ijumaa kuonyesha kuunga mkono na heshima kwa jamii ya Waislam.

Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa maafisa wa polisi wanawake wanaofanya doria waliva skafu kichwani na kuvaa maua ya wardi juu ya vazi lao la kazi.

Kabla ya Imam kuzungumza kulikuwa na adhana ya kuwaita watu katika sala katika uwanja huo iliyotangazwa mubashara kupitia radio na televisheni nchi nzima.

Dakika mbili za kukaa kimya zilifuatiwa na adhana kwa kuwakumbuka wale wote waliouawa msikitini.

Ardern amesema baada ya adhana: “New Zealand inaomboleza vifo hiivi pamoja na nyie, sote ni kitu kimoja.”

Ardern amechukuwa hatua za haraka dhidi ya shambulizi la umwagaji damu ndani ya misikiti hiyo.

Ameweka mara moja marufuku ya silaha zote za kivita ikiwemo bunduki aina ya semi-automatic na automatic, na assault rifles.

Katazo hilo, ambalo Waziri Mkuu Ardern amelitangaza Alhamisi Wellington, ni pamoja na magazine ya bunduki yenye uwezo wa kubeba risasi nyingi, na vipuli vingine ambavyo vinaweza kubadilisha silaha ya kawaida aina ya rifle kuwa silaha ya kivita. Ardern amesema ameweka katazo hilo kuzuia urundikaji wa silaha na marufuku kamili juu ya silaha hizo itatekelezwa baada ya sheria mpya kuanza kutumika.

Ardern ametangaza pia ununuzi mkubwa katika utaratibu wa kuwahamasisha wamiliki wa silaha kama hizo zilizopigwa marufuku kuzisalimisha kwa vyombo vya dola. Amesema serikali inaweza kutumia hadi Dola milioni 140 kuzinunua silaha hizo zilizoko mikononi mwa raia ambao watakuwa tayari kuzisalimisha.

Sheria hii ikipitishwa haitawagusa jeshi na polisi wa nchi hiyo, kama ilivyo kampuni za kudhibiti wadudu. Jeshi la polisi la New Zealand limesema katika tovuti yao “kipindi cha mpito” kitawawezesha watu kurejesha silaha zao serikalini bila ya adhabu yeyote.

Bunge la New Zealand linatarajiwa kupitisha pendekezo la sheria hiyo litapokutana tena kati ya mwezi April.

Vyombo vya usalama vimemfungulia shtaka la mauaji mzaliwa wa Australia Brenton Harrison Tarrant, 28, linalofungamana na shambulizi la Machi 15 katika misikiti miwili ya al-Noor na Linwood.

Mtu huyu mwenye sera binafsi za ubaguzi dhidi ya wahamiaji na Waislam hakukiri makosa wakati alipofikishwa mahakamani siku ya pili baada ya shambulizi hilo. Atarudishwa tena mahakamani Aprili 5, 2019.

XS
SM
MD
LG