Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 18:08

Papa Francis akutana na Kiongozi Mkuu wa Shia Iraq


Papa Francis akiwasili kukutana na Kiongozi Mkuu wa dhehebu la Shia, Ayatollah Ali al-Sistani, huko Najaf, IrakiMarch 6, 2021. Picha kwa hisani ya Vatican Media/­kupitia REUTERS
Papa Francis akiwasili kukutana na Kiongozi Mkuu wa dhehebu la Shia, Ayatollah Ali al-Sistani, huko Najaf, IrakiMarch 6, 2021. Picha kwa hisani ya Vatican Media/­kupitia REUTERS

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Ulimwenguni, Papa Francis, amekutana Jumamosi mjini Iraq na Ayatollah Ali al-Sistani, kiongozi wa Kiislamu wa dhehebu la Kishia.

Kikao hicho cha kihistoria kati ya papa mwenye umri wa miaka 84 na al-Sistani anayeishi akifanya ibada peke yake kimefanyika katika makazi ya kawaida ya kiongozi wa Kiislam mwenye umri wa miaka 90 katika mji mtakatifu wa Najaf.

Al-Sistani amesema Wakristo wanahaki sawa kama Wairaki wengine na lazima waishi katika mazingira ya amani.

Al-Sistani ni mmoja wa viongozi muhimu sana katika dhehebu la Kiislam la Shia na anaushawishi mkubwa ndani ya Iraq na nje ya nchi hiyo.

Wakristo nchini Iraq wana matumaini maoni ya al-Sistani na ujumbe wa Francis wa watu kuishi kwa kuvumiliana utasaidia kurahisisha maisha yao katika nchi yenye Waislam wengi, ambapo wanajikuta mara nyingi wakishambuliwa na wanamgambo wafuasi wa dhehebu la Shia.

Papa Francis akiwa Iraq baada ya kuendesha inada.
Papa Francis akiwa Iraq baada ya kuendesha inada.

Kiongozi wa kidini mjini Najaf ameliambia shirika la habari la Associate Press kuwa “mkutano huo ulikuwa wa binafsi ambao haujawahi kufanyika, na haufanani na ziara zozote za awali.”

Kukutana kwa viongozi hao wawili wa kidini kumetokea wakati kukiwa na uwezekano wa shambulizi la roketi zinazo pigwa nchini Iraq kutoka kwa vikundi vinavyoungwa mkono na Iran na janga la dunia la COVID-19.

Baada ya kukutana na al-Sistani, Francis alihudhuria mkutano wa dini mseto katika mji mkongwe wa Ur ambako tena alitoa hotuba ya kusisitiza kuishi pamoja kwa amani.

“Kutoka sehemu hii, ambapo Imani ilizaliwa, kutoka katika ardhi ya baba yetu Ibrahim (Abraham), kwa pamoja tuthibitishe kuwa Mungu ni mwenye huruma na kufuru kubwa kuliko zote ni kutumia jina lake kueneza chuki kwa kaka na dada zetu,” Francis alisema.

Ur ni mahali ambapo inaaminika ndipo alipozaliwa Ibrahim (Abraham), mahali patakatifu kwa dini zote tatu- Uislam, Uyahudi na Ukristo.

Baadae leo Jumamosi Papa ataendesha ibada katika Kanisa la Chaldean la Mtakatifu Joseph mjini Baghdad.

Francis pia atatembelea miji ya Mosul, Erbil na Qaraqosh kabla ya kuondoka Iraq

Papa ataendesha ibada ya nje katika uwanja wa mpira wa Erbil Jumapili mchana. Kutokana na sheria za kudhibiti COVID-19, watu wataoruhusiwa kuhudhuria ibadha hiyo hawazidi 10,000.

Uwepo wa Wakristo nchini Iraq unarejea karne ya kwanza ya dini hiyo, lakini maelfu ya Wakristo wachache wangali wanaishi hadi leo.

Hii ni ziara ya papa ya 33 nje ya Italia na ya kwanza katika kipindi cha miezi 15 sababu kuu ikiwa ni COVID-19.

Papa amepangiwa kurejea Rome Jumatatu asubuhi.

XS
SM
MD
LG