Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 04:11

Wakristo kote duniani waadhimisha sikukuu ya Krismasi


Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis.
Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis.

Wakristo ulimwenguni kote Ijumaa walisherehekea sikukuu ya  Krismasi kama maadhimisho ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo aliyezaliwa zaidi ya miaka 2000 iliyopita, kwa mujibu wa wanahistoria.

Tofauti na miaka ya nyuma, sherehe za mwaka huu zimegubikwa na janga la COVID-19.

Hali hiyo imelazimu mabadiliko kwa namna sherehe mbalimbali zinavyofanyika, huku serikali za nchi nyingi, zikiweka masharti mabalimbali, na mamilioni ya watu kusalia majumbani.

Mapema Ijumaa, kiongozi mkuu wa kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis, alitoa wito kwa watu wote duniani kujali maslahi ya wenzao, katika kipindi hiki kigumu.

"Wakati ulimwengu ukikumbwa na athari na majanga ya kipekee, ni muhimu kwa kila mtu kumfikiria mwenzake, kama ndugu na dada, na kuwajali watu walio na mahitaji, katika jamii," alisema Baba Mtakatifu.

Alikuwa akiongoza ibada katika kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican, ambayo ilihudhuriwa na waumini wachache kuliko ilivyo kawaida, na ambayo ilipeperushwa moja kwa moja kwa njia ya mtandao.

Kwingineko, sehemu za ibada zilikuwa na waumini wachache huku zikine zikisalia bila watu, wengi wao wakifuatilia ibada mitandaoni.

Shirika la habari la AFP linaripoti kwamba Korea Kusini, ni moja ya nchi ambazo zimeshuhudia kanisa nyingi zikiwa bila waumini.

Wafanyabiashara katika maeneo mbalimbali ulimwenguni wamenukuliwa na vyombo vya Habari wakilalamikia kushuka kwa biashara kutokana na athari za janga la Corona, katika msimu ambao, kwa kawaida, huwa wanashuhudia ongezeko kubwa la biashara.

Nchini Tanzania, Rais John Magufuli aliwataka wananchi kuendelea kumuomba Mungu alilinde taifa dhidi ya jangaa la Corona katika kipindi hiki ambacho mataifa mengine yanaendelea kuathiriwa na ugonjwa huo."

Rais wa Tanzania John Magufuli.
Rais wa Tanzania John Magufuli.

"Na pia nawaomba viongozi wa mataifa mbalimbali duniani kukubali kumweka Mungu mbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa huo badala ya kutegemea nguvu za binadamu pekee," aliongeza Rais Magufuli.

Kauli hiyo imekuja kipindi ambacho katika mataifa mengi ya Afrika na Ulaya, wengi wameshindwa kuhudhuria ibada ya krismasi kutokana na hofu ya kuambukizwa ugonjwa huo unaoendelea kusambaa katika mataifa hayo.

Kwingineko, rais wa Kenya Uhuru Kenyatta aliwatakia wananchi heri njema ya Krismasi na kueleza matumaini yake kwamba, licha ya changamoto zilizopo katika kipindi hiki, wataendelea kumuenzi Mwenyezi Mungu, na pia kujitahidi katika yote wafanyayo, ili kuhakikisha kwamba maisha yanaboreka kwelekea kwa mwaka mpya wa 2021.

Viongozi wengine mbalimbali katika ukanda wa maziwa makuu wamekuwa na kauli zinazofanana, wakiwatakia raia wa nchi zao heri njema ya Krismasi na mpya wa 2021.

Katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, sherehe ya Krismasi zilifanyika katika hali tulivu katika maeneo mabalimbali ya mji wa Bukavu, jimbo la Kivu Kusini, lich ya wakazi kulalamikia hali ngumu ya maisha wakati huu mgumu wa janga la Corona, na pia kupanda kwa bei ya vyakula.

-Mwandishi wetu wa Bukavu Mitima Delachance pia alichangia ripoti hii.

XS
SM
MD
LG