Kikundi hicho ni sehemu ya kikundi kidogo lakini inaongeza idadi ya wahamiaji kutoka nchi nyingine mbali na Mexico na Amerika ya Kati wanaovuka na kuingia kusini mwa Marekani bila kibali.
Wakati wengi wa watu ambao wanakamatwa na walinda doria mpakani Marekani katika mpaka wa Marekani na Mexico wanatokea Mexico, El Salvador, Guatemala na Honduras, wahamiaji kutoka nje ya nchi hizo idadi yao ni asilimia 4.3 ya jumla ya wahamiaji 303,916 waliokamatwa katika mwaka 2017, na asilimia 6.8 ya jumla ya wahamiaji 593,507 waliokamatwa kufikia mwaka 2019, kulingana na takwimu za serikali.
Wahamiaji kutoka Afrika
Kuanzia mwezi Mei, maafisa wa Forodha na Ulinzi wa Mpakani wa Marekani (USCBP) katika sekta moja huko Texas walikutana na vikundi vikubwa kadhaa vya wahamiaji, vikiwa na zaidi ya watu 100 kutoka nchi za Afrika, ikiwemo Jamhuri ya Congo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Somalia, Niger, Nigeria Angola na Cameroon.
“Pengine kwa zaidi ya miezi mitatu au minne iliyopita, tumeshuhudia ongezeko la wahamiaji kutoka bara la Afrika… na hili linaendelea kuwa ni tatizo kwetu,” Raul Ortiz, mkuu wa USCBP wa sekta ya Del Rio, ameiambia VOA.
Katika mwaka wa 2018, raia kutoka nchi hizo hizo zilizoorodheshwa awali 67 kati yao walikamatwa katika eneo lote la mpaka wa Marekani na Mexico, ukilinganisha na wengine 640 waliokamatwa katika wiki za hivi karibuni, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na USCBP na takwimu zilizopatikana kutoka ofisi ya Ortiz wiki iliyopita.
“Kitu kimojawapo kati ya vingine tunachofahamu ni kuwa wahamiaji hawa wengi wao wamekuwa wakisafiri kwa muda sasa – kati ya miezi minne na sita, Imesema Ortiz. Kwa sababu zozote zile, iwe niau makundi yanayofanya biashara haramu ya kusafirisha binadamu, imewaleta watu hao katika maeneo yetu ya uwajibikaji. Na hivyo tunaanza kuona na kukutana nao ndani na sehemu za mto wa nchi hii ambazo tunafanya doria.”
Ofisi ya Forodha na Ulinzi wa Mpakani ya Marekani inasema kuwa moja ya kikundi cha kwanza kilichoingia Marekani Mei 30 cha watu 116 kati yao 80 walikuwa wanatokea Congo, 35 Angola na mmoja Cameroon.
Siku ya pili yake, ofisi hiyo iliweka picha ya video ambayo ni rangi nyeusi na nyeupe ikionyesha kikundi kikivuka maji yenye urefu wa kufikia mapajani, baadhi ya watu wazima wakiwa wamewabeba watoto juu ya mabega yao.
Wasafiri katika makundi ya kifamilia
Takriban raia wa Africa wote waliokamatwa wamesafiri katika makundi ya kifamilia, Ortiz ameiambia VOA.
Kuwasili kwao kumesadifu wakati ambapo Marekani inakabiliana na idadi inayoongezeka ya wahamiaji haramu wanaovuka mpaka mwaka 2019, inayohamasishwa na shinikizo kwa familia hizo kuingia nchini na watoto wao wadogo.
Wakiwa na uzoefu wa kukutana zaidi na wanaozungumza lugha za kihispania na lugha asili za Amerika ya Kati, kuwasili kwa wanaozungumza Kifaransa na Kireno kutoka nchi za Kiafrika imefanya wafanyakazi na maafisa wa eneo kuanza kutafuta wakalimani.
Jiji la San Antonia katika Jimbo la Texas, karibu na mpaka wa Marekani na Mexico, lilitoa ombi kwa wanaozungumza Kifaransa kujitokeza na wiki iliyopita ilikuwa inapeleka wafanyakazi hao mpakani.
“Kumekuwa na wimbi kubwa la wahamiaji kuanzia jana [Jumatano] na wanaendelea kuingia, na tumeambiwa tutarajie wengine wengi,” amesema Christina Higgs, msemaji wa taasisi ya Catholic Charities San Antonio.
Wahamiaji zaidi wako njiani
Ortiz amesema pia kuwa sekta yake ya mpakani inategemea wahamiaji zaidi kuwasili, “hivi upande wa kusini wako wanaosubiri kuingia,” taarifa za kiintelijensia zimesema.
Hata hivyo sababu hasa za kuongezeka wanaovuka mpaka kutokea nchi za Kiafrika hazieleweki, hali ya machafuko ya kisiasa na vita katika nchi hizo kadhaa wanakotokea zinachangia. Kwa upande wa DRC, vita vya wenye kwa wenyewe vimesababisha watu milioni 4.5 kukimbia makazi yao ndani ya nchi na wengine takriban 800,000 kukimbilia nchi nyingine za Kiafrika, kwa mujibu wa Shirika la Wakimbizi la UN.
Na zaidi ya hilo, mwaka 2017 katazo la Wasomali kusafiri kuja Marekani lililotolewa na Marekani lilipelekea kupungua sana idadi ya visa zinazotolewa kwa wahamiaji na za wale wasiokuwa wahamiaji. Kupokelewa kwa wakimbizi ambao kwa miaka mingi walikuwemo maelfu ya Wasomali, idadi imepungua sana chini ya utawala wa Trump, ikiwa baadhi ya wasafiri hawana njia yeyote ya kuingia Marekani.