Mukundwa alikuwa ana miaka minane wakati alipolazimika kujificha katikati ya miili ya maiti, na hivyo kuwa mtu pekee katika familia aliyeweza kusalimika katika mauaji ya halaiki mwaka 1994 ambayo yaliigubika Rwanda, likiwemo eneo la Kibuye, Jimbo la Magharibi, ambako ni kwao. Anakumbuka mtu ambaye alimuuwa mama na kaka yake.
“Muuaji huyo mwanaume ndio aliyenikata miguu yangu kwa panga,” anasema Mukundwa, na majeraha yake yamefanyiwa upasuaji mara sita. Anakumbuka daktari mkarimu katika hospitali ya eneo aliyekuwa anamtibu majeraha yake na kumficha wakati mauaji ya kikabila yalipozagaa yakiwalenga zaidi watu wa kabila la Watutsi.
Na anakumbuka alivyokuwa akimuomba Mungu wakati wote mauaji yalipokuwa yanaendelea.
“Nilimwambia Mungu iwapo nitafanikiwa kuondoka sehemu hii nikiwa hai, nitatoa maisha yangu yote kuwasaidia watu wengine,” amesema.
Hivi sasa akiwa na miaka 33, Mukundwa ameweza kutekeleza mazuri katika ahadi yake aliyomuahidi Mola wake kupitia taasisi isiyokuwa ya kibiashara ya Safi Life ambayo aliianzisha. Kazi ya taasisi hiyo ni kuwaelimisha, kuwajengea uwezo na kuwasaidia wanawake vijana wa Rwanda kuweza kupiga hatua katika maisha yao.
Safi Life ilianzishwa rasmi mwaka 2012, ikakua kutokana na urafiki kati ya yule jina lake lilianzisha taasisi hiyo na Devon Ogden.
Wanawake hawa walikuwa wanafunzi chuoni wakati Ogden, Mmarekani kutoka California, alipotembelea Rwanda wakati wa msimu wa joto mwaka 2007 na kupata fursa ya kusikia ushahidi wake kwenye Kituo cha Kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbali Kigali. Walikutana kwa ajili ya chakula ya mchana, na Ogden ndipo alipomuuliza ni kwa namna gani ataweza kuwasaidia vijana wa Rwanda.
Mukundwa anakumbuka “nilimtaka anisaidie mimi ili niweze kuwasaidia wengine” kwa kutoa ufadhili wa masomo kwa wale walionusurika katika mauaji ya halaiki.
Ogden alianzisha taasisi ya kuwasaidia wasichana wa Rwanda na wanawake yenye makao yake Marekani, na Mukundwa akawa ni mkurugenzi wa taasisi ya Safi Life nchini Rwanda. Juhudi ya kwanza ya taasisi hiyo ilikuwa nikutoa ufadhili wa masomo kwa walionusurika katika mauaji ya halaiki.
“Hivi sasa tuna wasichana wawili wako shuleni wanasoma na tayari wamewawezesha wengine 12 ambao wamemaliza chuo,” Ogden amesema katika mahojiano ya simu hivi karibuni kutoka Los Angeles, ambako anafanya kazi ya uigizaji. “Wote wanaishi nchini Rwanda wakiiendeleza nchi yao.
Taasisi hiyo katika ukurusa wake wa Facebook( foundation’s Facebook page) inaonyesha picha za wahitimu wenye furaha waliomaliza masomo yao chuoni, akiwemo Florence, ambaye alitumia nafasi hiyo ya ufadhili wa masomo kusoma uhandisi wa madini. Ameweza kupata “kazi ya ndoto yake” akiwa ameajiriwa sasa na kampuni ya madini.
Mwaka 2018, Safi Life ilianzisha mradi wa jamii kusaidia wanawake vijana, hususan wale ambao hawajaolewa na ni wajawazito au tayari wana watoto wadogo.
Taasisi hiyo ilifungua kituo katika kitongoji cha Karembure mjini Kigali, na kuwakaribisha darzeni ya wanawake hao kuja kujifunza kufuma, kushona na ujuzi mwengine utakao wawezesha kutengeneza kipato.
Mradi huo, unaoitwa Ndashoboye, ambalo ni neno la Kinyarwanda lenye maana ya “Mimi ninaweza,” ambayo pia inatoa ushauri juu ya kuendesha biashara. Kituo cha pili kilifunguliwa Januari huko Ndera, kilomita chache kutoka mjini Kigali.
“Tunawasaidia wasichana wenye umri mdogo waliokuwa na watoto kwa kuwapa mafunzo ya ujuzi wa msingi kuwafanya wawe wanaweza kujitegemea na wanaweza kuwasimamia watoto wao wachanga” na kuishi maisha ya kuheshimika, Mukundwa anasema. “…Pia tunatoa ushauri nasaha kwao. Wengi wao wanakuja kwetu wakiwa na msongo wa mawazo uliovuka kiwango ambao na iwapo hawasaidiwa unaweza kupelekea maradhi ya akili.”
Mimba nje ya ndoa ni kitu kisichokubalika katika jamii ya nchi hii ya Afrika ya kati yenye wakazi milioni 12.3. Wasichana masikini ndio wanaoathirika zaidi, na mimba na uzazi wa utotoni ndio aghlabu unasababisha waache masomo.