Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 22:11

Hayati Mzee Mwinyi azikwa Zanzibar


Mazishi ya aliyekuwa rais wa awamu ya pili wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi.
Mazishi ya aliyekuwa rais wa awamu ya pili wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Jumamosi aliongoza maziko ya Rais mstaafu wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi yaliyofanyika kijijini kwake Mangapwani kisiwani Unguja na kuhudhuriwa na wananchi pamoja na viongozi kutoka nchi mbalimbali barani Afrika.

Wakati wa mazishi hayo, wengi walimkumbuka kwa mageuzi mbalimbali aliyoyafanya nchini humo.

Katika hotuba yake wakati wa mazishi hayo, Rais Samia alimtaja Rais Mwinyi kuwa ndiye Mtanzania wa kwanza kuwahi kuwa Rais Tanzania bara na visiwani na licha ya kupita katika vipindi vigumu vya kisiasa na kiuchumi alihakikisha kuwepo kwa utulivu na kufanya mageuzi makubwa katika nyanja mbalimbali.

"Yeye ndie Mtanzania wa kwanza kuwahi kuwa rais wa Zanzibar na baadaye rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pamoja na kupita katika vipindi vigumu kisiasa na kiuchumi, Rais Mwinyi aliweza kuhakikisha utulivu na kufanya mageuzi makubwa katika nyanja za kisiasa kijamii, kiuchumi kote Zanzibar na Tanzania" alisema Rais Samia.

Hayati Mwinyi alikuwa rais wa kwanza kuiongoza Tanzania baada ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 1984 yaliyojumuisha haki za binadamu kwenye katiba na hivyo kuwa Rais wa kwanza kuiongoza serikali inayozingatia haki za binadamu na utawala bora.

Ayubu Juma kutoka Lushoto anamkumbuka Rais Mwinyi kwa namna alivyokuwa mpole na mnyenyekevu na hivyo anawaasa viongozi waliobakia kufuata nyayo za Rais huyo kwakuwa wapole na wanyenyekevu mbele ya wananchi.

"Wito wangu kwa viongozi ambao wapo na watakaokuja kitu kikubwa kwa mzee Mwinyi alikuwa ni mpole na mvumilivu kwahiyo ninachowashauri viongozi ni kujaribu kuwa wapole na kujaribu kuangalia kuwa wananchi wakati mwingine wanahitaji kubembelezwa kuliko kutumia nguvu nyingi" alisema Juma.

Aidha Hayati Rais Mwinyi anakumbukwa zaidi kuwa ndie Rais wa kwanza kuleta mageuzi katika nyanja ya biashara na kuruhusu uwekezaji kutoka sekta binafsi na kupelekea kuleta ahueni ya maisha kwa wakati huo.

Fatuma Ally kutoka Tanga anasema atamkumbuka Rais Mwinyi kwa kuwatoa katika hali mbaya ya kiuchumi, katika kipindi ambacho nguo za kuvaa zilikuwa hazipatikani lakini kutokana na sera za Rais Mwinyi ikapelekea ahueni kupatikana.

Amesema Ally : "Alitutoa kwenye mambo magumu kwanza ilikuwa hatuvai nguo ipasavyo, nguo zilikuwa ghali na hazipatikani lakini tunashukuru alipoanza kutawala yeye kuna mambo mengi tuliyapata kwanza nguo za mitumba, pili tulikuwa hatuna runinga lakini tulizipata, sukari tulikuwa tunatumia guru lakini tulipata sukari ya kawaida kwenye utawala wake pamoja na simu".

Hayati Rais Mwinyi aliyefariki tarehe 29 akiwa na umri wa miaka 98 ameacha wake wawili Sitti Mwinyi na Khadija Mwinyi pamoja na watoto na wajukuu.

-Imeandaliwa na Amri Ramadhani, Sauti ya Amerika, Dar es Salaam.

Forum

XS
SM
MD
LG