Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 19:45

Changamoto zinazo walazimisha watoto kuacha masomo Sudan


Watoto wanavyotafuta ajira kutokana na umaskini
Watoto wanavyotafuta ajira kutokana na umaskini

Mamilioni ya watoto wa Sudan huondoka nyumbani kutafuta ajira kila siku badala ya kuhudhuria masomo, kutokana na umasikini uliokithiri na pili mfumo wa elimu usiyo na rasilmali za kutosha kuweza kuwahudumia.

Murtada Al Haj mwenye umri wa miaka 15 aliacha masomo miaka mitatu iliyopita ili kuitafutia familia yake riziki.

Murtada anaishi na wazazi wake mjini Khartoum huku akiwa na kipato cha chini ya dola 4 kwa siku, hali inayomzuia kutekeleza ndoto yake ya kuwa daktari.

Al Haj, Mfanyakazi mtoto anaeleza : "Mama yangu daima amekuwa akiniambia kwamba katika siku za mbele na ikiwa maisha yatabadilika na kuwa bora zaidi, basi nitasoma na kuwa daktari, lakini ghafla hali ya kisiasa iligeuka hapa Sudan.

Umasikini ulivyokithiri Sudan

Sudan imeorodheshwa kama mojawapo ya mataifa masikini zaidi duniani.

Kupanda kwa bei za bidhaa kulipelekea maandamano kote nchini yaliomuondoa madarakani Rais wa zamani Omar Al-Bashir mwaka 2019.

Licha ya hali ya kisiasa kutulia, uchumi ungali unasusua. Mjini Khartoum, ni kawaida kuona watoto wadogo wakifanya kazi za useremala, ufuaji chuma pamoja na biashara wakati wakipata kati ya dola moja na moja na nusu kwa siku.

Watoto wanalazimika kufanya kazi

Kwa Al Haj na maelfu ya wenzake, wanalazimika kuchagua kati ya kuhudhuria shule au kutafutia familia zao riziki. Hamza mmiliki karakana anasema hawana budi kuwasaidia.

Hamza anasema : "Watoto kutoka mitaa ya karibu hawawezi kuendelea na masomo kutokana na hali ngumu ya maisha. Baba zao huwaleta hapa ili tuwatafutie cha kufanya kutokana na ugumu wa maisha. Hata hivyo siyo wengi ambao huvumilia hali hii. Murtada kwa upande wake amevumilia kutokana na kuwa anaishi karibu hapa na pia kutokana na hali ngumu ya maisha anayopitia."

Maafisa wa serikali ya Sudan wametia saini mikataba ya kimataifa ya kutoa elimu ya bure kwa watoto pamoja na kusitisha ajira za watoto, lakini sheria hizo hazijatiliwa mkazo anasema Siddiga Kibeida mfuatiliaji haki za watoto.

Kibeida : "Umasikini ulioko Sudan unaathari kubwa kiasi cha kutoweza kuzuia ajira za watoto ingawa kuna sheria inayowazuia kufanya kazi kabla ya kutimiza umri wa miaka 18. Kudhibiti Umasikini ni suala muhimu kabisa."

Utafiti uliofanywa na wizara na Unicef

Utafiti uliofanywa na Wizara ya Elimu kwa ushirikiano na UNICEF umebaini kuwa zaidi ya watoto milioni 3 hawahudhurii masomo nchini Sudan. Waziri wa Elimu Mohammed el Amin anasema watoto wa umri wa Murtada hawana nafasi ya kuhudhuria shule.

Waziri wa Elimu anaeleza : "Nchi hii haiwezi kutekeleza haki za watoto. Ilichofanya ni kuweka mfumo wenye uwezo wa kusaidia asilimia 60 ya watoto pekee huku asilimia 40 wakibaki bila nafasi ya kupata masomo na hiyo ndiyo sababu kubwa ya kuwa na watoto milioni 3 ambao hawahudhurii masosmo kulingana na ripoti ya UNICEF."

Kutokana na kuwepo na serikali mpya, Murtada ana matumaini kwamba mfumo wa elimu utabadilika ili apate nafasi ya kwenda shule na kutimiza ndoto yake ya kuwa daktari.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Harrison Kamau, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG