Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 22:05

Chadema Yamuunga mkono Maalim Seif wa ACT urais Zanzibar


Maalim Seif Sharif Hamad
Maalim Seif Sharif Hamad

Hii itakuwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa 2020 Tanzania kwa vyama vya upinzani kuwa na ushirikiano nyuma ya mgombea mmoja.

Chama cha upinzani cha Chadema nchini Tanzania kimetangaza Jumatatu Zanzibar kuwa kinamuunga mkono mgombea urais wa chama cha ACT Wazalendo katika kinyang’anyiro cha urais visiwani humo.

Akihutubia mkutano wa kampeni mjini Unguja mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia Chadema, Tundu Lissu, amesema Maalim Seif Shariff Hamad wa ACT ndio mgombea pekee ambaye anaweza kuishinda CCM Zanzibar.

Tundu Lissu
Tundu Lissu

“Mtu pekee na chama pekee chenye uwezo wa kuishinda CCM Zanzibar, kiongozi wa Wazanzibari, ni Maalim Seif. Huyo ndiye mtu ambaye sisi Chadema tutamuunga mkono,” alisema Lissu.

Ingawa hakusema moja kwa moja kwamba Chadema inamwondoa mgombea wake Zanzibar Said Issa Mohammed katika kinyang’anyiro hicho, matamshi ya Lissu yana maanisha kuwa Chadema haitamnadi mgombea huyo na badala yake itaungana na ACT Wazalendo kumnadi Maalim Seif katika kuwania urais wa Zanzibar.

Mgombea urais wa chama tawala cha CCM Zanzibar ni Dkt Hussein Mwinyi ambaye alikuwa Waziri wa Ulinzi katika awamu ya kwanza ya Rais John Pombe Magufuli katika Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Kampeni za uchaguzi wa urais na wabunge Zanzibar zinaanza rasmi Septemba 11.

Dr Hussein Mwinyi akihutubia mkutano mkuu wa CCM Dodoma, Tanzania wakati akikubali kugombea nafasi ya urais Zanzibar kwa tiketi ya chama chake Agosti 2020.
Dr Hussein Mwinyi akihutubia mkutano mkuu wa CCM Dodoma, Tanzania wakati akikubali kugombea nafasi ya urais Zanzibar kwa tiketi ya chama chake Agosti 2020.

Katika mkutano wake wa kwanza wa uchaguzi Zanzibar, Lissu alisema Maalim Seif na wenzake wamekuwa sauti kuu ya upinzani Zanzibar kwa karibu miaka 35 kuitetea Zanzibar na maslahi yake.

“Hajawahi kubadilisha msimamo. Alianza akiwa kijana, leo ni mzee lakini msimamo wake juu ya Zanzibar haujatetereka. Huyo ndio mtu ambaye anayeweza kuishinda CCM Zanzibar na huyo ndio mtu ambaye sisi Chadema tutamuunga mkono,” alisema Lissu.

XS
SM
MD
LG