Kupitia taarifa iliyotolewa Jumapili, Zitto Kabwe pia ameishutumu tume ya uchaguzi ya Zanzibar kwa kuwabagua wafuasi wa upinzani na kusema kwamba iwapo vitendo hivyo vitaendelea bila kudhibitiwa, itakuwa ni vigumu kuwa na uchaguzi huru na wa haki.
Kabwe amesema kwamba amani na utulivu wa Tanzania uko mikononi mwa taasisi hizo, na kwamba kama hakuna wagombea, basi hakuwezi kuwa na uchaguzi.
Ameongeza kwamba taasisi hizo zinapendelea chama kinachotawala cha CCM.
Alikuwa akizungumzia mchakato wa kuidhinisha uteuzi wa wagombea wa ubunge na udiwani ambao umeibua utata na kukosolewa na wapinzani na makundi ya kutetea haki za kiraia, kwamba ulitumiwa kuwaengua wafuasi au wagombea kutoka kwa vyama vya upinzani.
Kabwe ameorodhesha mbinu kadhaa, ambazo amesema zilitumiwa na tume hizo kuwaengua wagombea wa upinzani, akitoa mfano wa Zanzibar, ambako ni wagombea 14 tu wa chama hicho ambao waliidhinishwa, kati ya jumla ya wagombea 50.
Ametaka walioenguliwa waidhinishwe na tume hizo na kusema kwamba chama chake kiko tayari kutumia mbinu mbalimbali kushinikiza mamlaka husika kuwatendea haki wafuasi wake.
Aidha Kabwe amesema Inspekta Mkuu wa Polisi Simon Sirro alitembelea kisiwa cha pemba tarehe nne mwezi huu wa Septemba na kuwatishia wakazi "kwa kisingizio kwamba alikuwa anashinikiza" amani.
"Tungependa kumkumbusha Inspekta Sirro kwamba amani hutokana na haki," amesema Kabwe.
"Iwapo wagombea wetu watashambuliwa, tuatatumia nguvu ya umma kuhakikisha kwamba haki imetendeka na sisi tutakuwa kwenye msitari wa mbele katika msukumo huo," ameongeza.