Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 16:22

CCM yamfukuza Membe, Kinana akaripiwa na Makamba asamehewa


Yusuf Makamba (kushoto), Bernard Membe (Kati) na Abdulrahman Kinana (kulia).
Yusuf Makamba (kushoto), Bernard Membe (Kati) na Abdulrahman Kinana (kulia).

Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC), imetoa adhabu ya kumfukuza uanachama aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika serikali ya awamu nne, Bernard Membe kutokana na madai ya kuwa alikiuka maadili ya chama hicho.

Viongozi wengine wa ngazi ya juu wa zamani wawili ambao walitumikia nafasi ya katibu mkuu wa chama Yusuf Makamba amesamehewa na Abdulrahman Kinana amepewa onyo..

Akizungumza na waandishi wa habari ofisi ndogo za chama hicho Dar es Salaam, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ,NEC, (Itikadi na Uenezi), Humphrey Polepole, amesema Kamati Kuu iliyoketi chini ya Mwenyekiti wa Taifa Rais John Magufuli ilifikia uamuzi huo.

Polepole amesema mwaka 2014 Membe alikuwa miongoni mwa makada sita wa chama cha Mapinduzi CCM waliofungiwa kwa kipindi cha miezi 12 kutojihusisha na siasa katika chama hicho, baada ya kubainika kufanya makosa ya kimaadili kutokana na kuanza mapema kampeni za urais kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Polepole ameongeza kuwa Kamati Kuu pia imempa karipio Katibu Mkuu Mstaafu, Abdulrahman Kinana ambapo kwa mujibu wa kanuni za CCM mwanachama anayepewa adhabu ya karipio anakuwa chini ya uangalizi kwa kipindi cha miezi 18, huku akizuiwa kutojihusisha kugombea nafasi yoyote ndani ya chama hicho.

Kamati Kuu pia imetoa msamaha kwa kada wake mwingine, Yusuph Makamba ambaye naye ni katibu mkuu mstaafu, baada ya mzee Makamba kuomba msamaha kwa maandishi juu ya makosa yake ya kimaadili.

Polepole amesema mbali ya ajenda hiyo Kamati Kuu pia ilijadili ajenda nyingine ikiwemo, kasi ya maambukizi ya virusi vya Corona katika nchi mbalimbali duniani pamoja na tatizo la uvamizi wa Nzige waliopo katika nchi jirani, ambapo Kamati Kuu imeitaka Serikali kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na majanga hayo.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG