Akizungumza katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Jumatatu mjini Dar es Salaam, Kinana amesema “lazima tukubali kuna wakati wa kufanya kazi na kuna wakati wa kupumzika.”
Ameongeza kusema:”Naelewa ugumu mnaoupata wa kutonikubalia. Mnakubali tu Nnaelewa, kila nikiwatizama, nimepata message nyingi na hata nyuso zenu nikizitizama bado mnauliza kwamba je huwezi kubadili mawazo.”
“Na nyinyi ni mashahidi Mwenyekiti amesema kumekuwa na makatibu wakuu wengi tangu CCM izaliwe. Kumekuwa na makatibu wakuu saba kwa hiyo sio ajabu na katibu mkuu wa sasa akiachia ngazi, apatikane katibu mkuu mwengine.”
Akipokea ombi hilo la kustaafu, Mwenyekiti wa CCM, John Magufuli amekubali ombi la Kinana.
“Huyu kweli ameshaomba zaidi ya mara mbili. Na zile nyingine alikuwa anaomba kisiri siri namkatalia, akiweka neno hilo naanzisha neno jingine.”
Magufuli ameongeza kuwa “Lakini nikatambua pia juhudi kubwa. Kwa kujiuliza kwa kusema ni makatibu wakuu wangapi wamekuwa tangu tupate uhuru? Nikajua walikuwepo hata mimi bado sijaanza shule ya msingi, amesema.
Magufuli amesema kuwa kila katibu mkuu alianza kazi yake akamaliza wakati wake.
“Lakini pia nikatambua umri wa mheshimiwa Kinana, nikazungumza na Mzee Shein, akaniambia kwa kweli tumkubalie,” amefafanua.
Kwa upande wake Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, amesema kwa pamoja wamemtakia mafanikio mema katika shughuli zake.
“Napenda kumshukuru ndugu Kinana kwa utumishi wake katika Chama cha Mapinduzi (CCM) na CCM itaendelea kutumia uzoefu wake katika majukumu mbalimbali ya chama kwa kadiri itakavyohitajika", imesema taarifa iliyotolewa na CCM.