Mazungumzo yao yamejiri juu ya maandalizi ya vikao vya Kamati Kuu ya CCM (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) vitakavyofanyika tarehe 28-29, Mei, 2018 mjini Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu pia imesema kuwa Magufuli alipokea salamu kutoka kwa viongozi wa chama na serikali wa Afrika Kusini na Zimbabwe ambako hivi karibuni Kinana aliongoza ujumbe wa viongozi wa CCM kutembelea nchi hizo na kukutana na viongozi wakuu wa vyama tawala vya ANC na ZANU - PF vinavyoongoza serikali.
Wakati huohuo msemaji wa CCM amesema kuwa mpaka Jumapili hakupokea barua yoyote au taarifa rasmi juu ya kujiuzulu kwa Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana.
Akizungumza na Global TV nchini Tanzania Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Humphrey Polepole, amesema habari hizo ni za uzushi.
Katika habari zilizochapishwa na baadhi ya magazeti nchini ziliripoti kuwa Kinana amemwandikia barua Mwenyekiti wa chama hicho, akimuomba kujiuzulu wadhifa wake huo.
Kinana ametumikia nafasi ya Katibu Mkuu wa CCM tangu mwaka 2012. Julai 2016, katika Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM ambao Rais mstaafu Jakaya Kikwete alimkabidhi uenyekiti wa CCM Rais Magufuli, ikiwa ni miezi minane tangu aingie madarakani,
Kinana aliwasilisha barua ya kujiuzulu nafasi hiyo, lakini kiongozi huyo wa nchi aliikataa akimwomba amsaidie kwa sababu ya uzoefu wake.
Rais Magufuli, pia aliwataka manaibu katibu wakuu wawili na sekretarieti nzima ya chama hicho, kuendelea na kazi.