Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 19:52

Tanzania : Miaka miwili yapita tangu kupotea Azory Gwanda


Wafanyakazi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited, wadau wa habari na familia ya Azory Gwanda wakishiriki katika zoezi la kupanda mti kama ishara ya kumkumbuka na heshima kwa mwandishi Azory Gwanda. Picha kwa Hisani ya Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd, Tanzania
Wafanyakazi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited, wadau wa habari na familia ya Azory Gwanda wakishiriki katika zoezi la kupanda mti kama ishara ya kumkumbuka na heshima kwa mwandishi Azory Gwanda. Picha kwa Hisani ya Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd, Tanzania

Mwandishi wa habari Azory Gwanda nchini Tanzania, aliyetoweka kwa kutekwa na watu wasiojulikana amekumbukwa Alhamisi na wafanyakazi wenzake, wadau wengine wa habari na familia yake nchini Tanzania.

Kampuni ya Mwananchi Communications Limited aliyokuwa akiitumikia imepanda mti na kuzindua picha maalumu kama ishara ya kumkumbuka na heshima kwa mwandishi wake Azory Gwanda.

Matukio hayo mawili yakumkumbuka na kumuenzi Azory yamefanyika Alhamisi ikiwa ni miaka miwili kamili tangu Azory kutoweka katika mazingira ya kutatanisha baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana akiwa anaripoti habari za mauaji yaliyokuwa yakitokea Wilaya Kibiti mkoa wa Pwani.

Kwa mujibu mwandishi wa VOA shughuli za kupanda mti na kuzindua picha maalumu ziliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi, Francis Nanai ambaye amesema kwamba kampuni inamkumbuka Azory kama mwandishi mahiri na jasiri ambaye alithubutu kuendelea na kazi yake hata katika mazingira ambayo yalikuwa na changamoto nyingi.

Naye mwandishi wa habari wa Mwananchi ambaye aliongea kwa niaba ya waandishi wa habari wengine wa kampuni hiyo, Dk Tumaini Msowoya aliiomba serikali kuongeza juhudi za kumtafuta Azory na kusisitiza kwa waandishi wengine kuzingatia weledi katika kazi zao na kuzifanya bila woga.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa mtu wa karibu wa mwisho kumuona alikuwa mke wake Ana Pinoni. Gwanda alikwenda shambani na kumkabidhi ufunguo wa nyumba Pinoni na kumueleza kuwa anaenda kazini.

Gwanda alikuwa ameongozana na watu wanne waliokuwa kwenye gari ambayo mkewe Pinoni anaitaja kuwa nia aina ya Toyota Land Cruiser yenye rangi nyeupe. Tangu wakati huo Azory Gwanda hajaonekana tena mpaka hii leo.

Baadhi ya wadadisi wamedai kuwa watu waliomchukua mwanahabari huyo ni maafisa usalama, jambo ambalo serikali ya Tanzania imelipinga.

XS
SM
MD
LG