Zoezi la maafisa wa jeshi la Marekani kutoa ushahidi bungeni laendelea

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin akitoa ushahidi mbele ya jopo la kamati ya bunge kuhusu kumalizika kwa operesheni ya miongo miwili katika bunge la Marekani, Washington, Sept. 28, 2021.(AP Photo/Patrick Semansky, Pool).

Maafisa wa ngazi ya juu wa jeshi la Marekani wanarudi bungeni Jumatano kutoa ushahidi mbele ya jopo jingine la kamati ya bunge kuhusu kumalizika kwa operesheni ya miongo miwili.

Hilo linajiri siku moja baada ya kutoa tathmini yao ya kumalizika kwa vita nchini Afghanistan, na vitisho vya ugaidi vya siku zijazo ambavyo vinaweza kutokea nchini humo.

Waziri wa Ulinzi Marekani, Lloyd Austin, mwenyekiti wa pamoja wa wakuu wa majeshi, Jenerali Mark Milley na Jenerali Keneth Frank McKenzie, kamanda wa komandi kuu ya Marekani, wote wanatakiwa kufika mbele ya kamati ya bunge inayohusika na huduma za jeshi.

Kwenye kikao cha Jumanne, mbele ya kamati ya Seneti, wabunge wote walisifu uamuzi wa kumaliza vita virefu zaidi nchini Marekani, na walilaani siku za mwisho za vita hivyo namna vilivyomalizika.

Austin alitetea uokoaji huo akisema kuwa ingawa sio kamilifu lakini ulikwenda vyema kadri iwezekanavyo na kwamba hakuna jeshi jingine ambalo lingefanya vizuri zaidi.