Wanawake nchini Afghanistan wanaweza kuendelea kusoma katika vyuo vikuu na hata baada ya kuhitimu, lakini vyumba vya madarasa vitatengwa kufuatana na jinsia pamoja na mavazi ya kiislamu ni lazima. Waziri wa elimu ya juu katika serikali mpya ya Taliban alisema Jumapili.
Waziri Abdul Baqi Haqqani alielezea sera mpya katika mkutano wa waandishi wa habari siku kadhaa baada ya watawala wapya wa Afghanistan kuunda serikali yenye wanaume watupu. Dunia imekuwa ikiangalia kwa karibu kuona ni kwa kiwango gani Taliban inaweza kuchukua hatua tofauti kutoka kipindi chao cha kwanza madarakani mwishoni mwa miaka ya 1990. Wakati wa enzi hizo, wasichana na wanawake walikataliwa elimu, na walitengwa kutoka maisha ya umma.
Taliban wanaeleza wamebadilika ikiwemo mitazamo yao kwa wanawake. Hata hivyo wamefanya ghasia katika siku za karibuni dhidi ya waandamanaji wanawake wanaodai haki sawa.