Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kukutana kujadili maendeleo hayo, wakati Marekani na zaidi ya nchi nyingine 60 zilitoa taarifa zikitaka pande zote nchini Afghanistan kuwaruhusu raia wa Afghanistan au wa kigeni kuondoka nchini humo ikiwa wanataka.
Marekani ilituma wanajeshi zaidi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kabul wa Hamid Karzai kusaidia kuwaondoa wanadiplomasia wa Marekani na washirika wa Afghanistan. Mataifa mengine ya Magharibi pia yalifanya kazi Jumatatu kuwatoa wafanyakazi wao nje ya nchi hiyo.
Maelfu ya raia wa Afghanistan pia wamejazana kwenye uwanja wa ndege, wakihofia kurudi kwa utawala wa Taliban lakini wanakabiliwa na njia isiyo wazi ya kutoka.
Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Afghanistan ilitoa taarifa leo Jumatatu asubuhi ikisema upande wa raia wa uwanja wa ndege umefungwa hadi hapo itakapotangazwa tena.