Jumamosi ilikuwa imekamilisha wiki ya 22 mfululizo za maandamano yanayoshinikiza kuwepo demokrasia yanayoendelea mitaani.
Siku ya Ijumaa, Shen Chunyaok, mkurugenzi wa jiji la Hong Kong, Macao na Kamisheni ya Sheria ameonya kuwa China “haiwezi kabisa kuruhusu mwenendo wowote unaunga mkono kujitenga kwa Hong Kong au kuhatarisha usalama wa taifa na itaendelea kuepusha hilo lisitokee. Pia itadhibiti hali yoyote ya mataifa yenye nguvu ya kigeni kuingilia masuala ya ndani ya Hong Kong na Macao na vitendo vyao vya kuchochea wananchi kujitenga, uasi, ujasusi na hujuma.”
Mwandamanaji mwenye umri wa miaka 18 Gordon Tsoi ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP : “Serikali na polisi wamekuwa wakibeza na kukandamiza madai ya wananchi hivyo inatulazimu kuendeleza harakati hizi kuwaonyesha bado tunataka kile tunachodai kwao.”
Kituo hicho cha fedha cha bara la Asia kimekumbwa na maandamano makubwa na yenye vurugu tangu Juni, yaliyosababishwa na pendekezo la muswada ambao ungeruhusu wanaoshukiwa kuwa wahalifu kusalimishwa China bara kufunguliwa mashtaka.
Maandamano hayo yamegeuka kuwa ni madai ya kuwepo demokrasia kamili Hong Kong, uchunguzi huru juu ya polisi kutumia nguvu kupita kiasi na msamaha kwa wanaharakati wote waliokamatwa wakati wa maandamano.
Waandamanaji waliofunika sura zao waliharibu maeneo ya biashara na miundo mbinu ya usafiri wa jiji hilo, na kuwashambulia polisi kwa matofali na mabomu waliotengeneza nyumbani kwa petrol.
Hong Kong ilikuwa inafurahia kiwango cha juu ya kujitawala chini ya “serikali moja lakini mifumo miwili ya utawala” katika utaratibu uliokuwepo wakati China ilirejeshewa Hong Kong ambayo ilikuwa chini ya Uingereza hadi mwaka 1997.