Ameonya kutokea janga hili ikiwa fursa za kufikisha msaada katika eneo hilo la kaskazini mwa nchi la Tigray, hazitaboreshwa kwa haraka, na misaada pamoja na ufadhili kuongezeka ipasavyo.
Mark Lowcock, ameuambia mkutano wa faragha, usio rasmi, wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, UN, kwamba utawala wa Tigray umeripoti vifo vingi, kutokana na njaa, na kuongeza kuwa hali itazidi kuwa mbaya katika miezi ijayo, sio tu huko Tigray, lakini pia katika majimbo ya Afar na Amhara.
Idara ya uainishaji wa awamu Jumuishi ya Usalama wa Chakula, au IPC, iliripoti kuwa zaidi ya watu milioni 5.5 kwa jumla walikuwa katika viwango vya mzozo wa ukosefu wa chakula katika jimbo la Tigray, na maeneo jirani ya Amhara na Afar.
Shirika la kuwahudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, pia limetahadharisha kuwa watoto 33,000 wenye utapiamlo wa kiwango cha juu katika maeneo yasiyofikika ya Tigray wako katika hatari kubwa ya kufariki.