Tweet za Balozi wa Marekani Kenya dhidi ya ufisadi zazua gumzo mtandaoni

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta (kushoto) akiwa na Makamu wake William Ruto, kulia Ikulu ya Nairobi, Kenya, Sept. 21, 2017.

Hivi karibuni Balozi wa Marekani nchini Kenya Kyle McCarter alisababisha mjadala mkubwa kwa wadau wa lugha ya Kiswahili alipotuma ujumbe wake wa Tweet kwa Wakenya katika Kiswahli fasaha na kuzua gumzo mtandaoni.

Alituma ujumbe huo kuwaeleza wananchi wa Kenya alivyo na furaha kutumikia nafasi hiyo yenye changamoto mpya na kueleza dhamiri yake ya kushirikiana na Serikali ya Kenya kwa ajili ya kuleta maendeleo.

Baada ya kukabidhi utambulisho wake kwa Rais Uhuru Kenyatta, ikiwa yuko tayari kuanza majukumu yake rasmi bega kwa bega aliandika ujumbe Machi 12, 2019, katika tweet, “Tutafanya kazi pamoja”

Lakini wiki iliyofuatia Balozi McCarter alituma ujumbe mwengine wa Kiswahili na kuanzisha mjadala. Hakuwa tu amejaribu kutumia Kiswahili cha kawaida lakini alitumia lugha iliyokuwa imechanganyika na lugha ya Sheng- ya wenyeji - kutaka kukonga nyoyo za watu wa Kenya kwamba anafahamu utamaduni wao.

Katika kuuelezea ufisadi alisema : “Corruption - ni Kama mbwa kubwa na nono. Anakuja Kwa Boma lako kila siku, anaingia ndani ya ghala lako na kukula chakula chako. Unampapasa kisha anaenda kwa boma nyingine. Na wananchi wanashangaa kwa nini wako na njaa. Lakini kama Thievery, mbwa huyo angekuwa Mg’ondi, mngemfukuza!”

Kilichofuatia ni mjadala ulioanzishwa na wafuasi wa tweet zake wengine wakimpongeza na baadhi yao wakisahihisha sentensi za ujumbe wake.

Wakili wa Nairobi Ahmednassir Abdullahi alituma ujumbe kwa balozi akisema: “Ni ukweli, uwazi , uaminifu, ujumbe wa moja kwa moja bila ya kumumusa maneno japokuwa inauma Bwana Balozi...”

Ali 'Mwamvita' Manzu alimjibu kwa kusema : “Bwana Balozi, nina uhakika umeandikiwa au umebadili kupitia mtandao wa Google, hata hivyo si vibaya. Ila ilivyo sahihi, Mbwa mkubwa wala sio mbwa kubwa. Jibwa ndio kubwa. Samahani ila lazima urekebishwe kwa matumizi bora ya lugha na isiwe bora lugha. Kumradhi.”

Ali Manzu, ambaye ni mtangazaji wa Kituo cha televisheni cha KTN alisisitiza kumwambia mwanadiplomasia huyo kuwa Kiswahili kama vile lugha nyingine inataka uwe na ufasaha na siyo ilimuradi kuzungumza.

“Ninajaribu kwa uwezo wangu wote kujifunza kutoka kwa marafiki zangu. Mimi sijakuwa fasaha. Ili kuweza kutuma ujumbe huu kwa Kiswahili, pamoja na mapungufu, baadhi ya malengo ni muhimu. Kufahamu majibu yote ni changamoto, lakini itabidi nifanyie kazi haya yote,” amesema McCarter katika majibu yake.

Hili lilikuja siku kadhaa baada ya ujumbe wake wa tweet wenye masahara Mei 30, 2019, kuhusu hafla ya Chai ya Asubuhi ya Maombi ya Taifa.

Alisema : Viongozi wa Kenya wanaomba na kutaka msamaha kwa madhambi ya wizi katika Maombi ya Taifa ya 17 ya Chai ya Asubuhi ya kila mwaka. Kwa hakika ni mwanzo mzuri kwa taifa kuelekea katika mafanikio ambayo wananchi wanastahili kuyapata. Kila moja lazima atekeleze jukumu lake. #stopthesethieves.”

Ikiambatana na ujumbe huu wa Balozi ilikuwa ni picha ya video ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto na viongozi wengine wakicheza huku wameshika fimbo, wakiwemo morani wa Kimasai wakati wananchi wakishangilia.

Mara nyingine tena balozi alikuwa katika mjadala na mchambuzi wa kisiasa Makau Mutua alipomtahadharisha kuwa asije akadanganywa.

“Balozi usifanywe mjinga. Wanafanya hili kila mwaka na hawachukui hatua yoyote. Huku ni kuonyesha unafiki kamili. Wengi walioko katika picha hiyo walitakiwa wawe jela kwa kile unachokiita “wizi,” Prof Mutua alituma tweet na kuongeza :

Balozi kile unachoshuhudia katika ngoma za msafara wa wezi tafrija ya udanganyifu. Inanikumbusha kikundi cha mashetani cha wanga na waovu wanaouzingira mzoga, katika hali hii, ikiwa ni Kenya.