Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 23:12

Serikali ya Kenya kutaifisha shirika la ndege la Kenya Airways KQ


Ndege ya shirika la ndege la Kenya Airways ikitua Nairobi, Kenya
Ndege ya shirika la ndege la Kenya Airways ikitua Nairobi, Kenya

Serikali ya Kenya inamiliki asilimia 48.9 ya hisa za shirika hilo ambalo limekuwa likipata hasara kila mwaka wa kifedha. Wabunge hata hivyo wametofautiana kuhusu jinsi ya kulipa madeni ya KQ, baadhi wakisema wananchi walipa kodi hawastahili kugharamia makosa ya usimamizi yaliyofanywa na watu binafsi

Mchakato wa kulitaifisha shirika la ndege la Kenya airways (KQ), umeanza rasmi, baada ya bunge la nchi hiyo kupitisha kwa pamoja ripoti ya kamati ya uchukuzi inayotaka serikali kusimamia shirika hilo.

Kupitishwa kwa ripoti hiyo kuna maana kwamba serikali ya Kenya italazimika kulipa madeni yote ya shirika la ndege la Kenya airways kabla ya kutaifishwa.

Hatua ya kulitaifisha shirika la ndege la Kenya airways, inachukuliwa ili kulinusuru na madeni yanayoendelea kuongezeka.

Serikali ya Kenya inamiliki asilimia 48.9 ya hisa za shirika la Kenya airways, ambalo limekuwa likipata hasara kila mwaka wa kifedha.

Shirika la Air france - KLM, linamiliki asilimia 7.8 ya hisa za shirika hilo la ndege. Asilimia 38.1 ya hisa inamilikiwa na kampuni zinazoikopesha Kenya airways.

Juhudi za kuinusuru KQ

Kenya Airways ilipendekeza kusimamia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta kwa muda wa miaka 30, ili kuimarisha mapato yake, baada ya kupata hasara ya dola bilioni 2 mwaka 2017, mpango uliokataliwa na kamati ya bunge kuhusu uchukuzi.

Kamati ya bunge badala yake ilipendekeza kwamba shirika hilo litaifishwe, katika ripoti iliyowasilishwa bungeni June 18.

Wabunge wa kenya wakiwa katika kikao cha bunge
Wabunge wa kenya wakiwa katika kikao cha bunge

Wabunge hata hivyo wametofautiana kuhusu jinsi ya kulipa madeni ya KQ, baadhi wakisema wananchi walipa kodi hawastahili kugharamia makosa ya usimamizi yaliyofanywa na watu binafsi, na kutaka wamiliki wa sasa wa hisa za shirika hilo kugharamia hasara. Baadaye wamekubaliana kwamba serikali itabeba mzigo wa kulipa madeni yote.

Mapendekezo mapya

Kupitishwa kwa ripoti hiyo ni hatua inayotoa fursa ya kuanza kwa mchakato wa kuangazia maslahi ya wafanyakazi wa KQ ikiwemo kusawazisha kiwango chao cha mishahara na majukumu yao jinsi ilivyopendekezwa katika ripoti.

Kenya Airways, litapata msamaha wa kulipa kodi kwa muda maalum ili kuiwezesha kutekeleza shughuli zake bila matatizo ya kifedha.

Ripoti pia inapendekeza kwamba mamlaka ya safari za anga KAA, Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta JKIA na shirika la ndege la KQ, viwekwe chini ya usimamizi mmoja.

Majibu ya wasimamizi wa KQ

Mwenyekiti wa shirika hilo Michael Joseph, katika mahojiano na shirika la habari la Reuters amesema hatua ya bunge ya kupitisha ripoti hiyo kuwa habari nzuri sana.

Ndege ya shirika la ndege la kenya Airways-KQ
Ndege ya shirika la ndege la kenya Airways-KQ

“utaifishaji ni muhimu sana ili tuweze kushindana kwa kiwango sawa. Sio tu tunachotaka, bali ni kitu tunachohitaji”, amesema Michael Joseph.

Amesema shirika la ndege la Ethiopia limefanikiwa pakubwa kwa sababu linasimamiwa na serikali.

Wasimamizi wa shirika la ndege la Air France –KLM, hawakuweza kupatikana wakati wa kutayarisha ripoti hii.

Katibu katika wizara ya uchukuzi ya Kenya Esther Koimett, amesema serikali sasa itaunda mpango wa utekelezaji.

XS
SM
MD
LG