Ushindi huu unamaliza vita kote nchini na unafungua njia kwa maisha ya amani na ustawi katika mazingira ya uhuru, msemaji wa Taliban, Zabihullah Mujahid alisema katika taarifa.
Timu ya habari ya Taliban, ilitoa kanda kadhaa za video za kuichukua Panjshir, na kupandisha bendera ya Taliban kwenye majengo ya serikali katika jimbo hilo hii leo.
Lakini vikosi vya upinzani vinavyojulikana kama “National Resistance Front”, vinavyoongozwa na kamanda Ahmad Massoud, vilikanusha madai ya Taliban katika ujumbe wa Facebook uliotumwa na Ali Maisam Nazary, mkuu wa masuala ya uhusiano wa mambo ya nje.
Katika chapisho hilo alisema madai ya Taliban ya kuikamata Panjshir, ni ya uongo.
Vikosi vya NRF vipo katika nafasi zote za kimkakati kote kwenye eneo ili kuendeleza mapigano.
Tunawahakikishia watu wa Afghanistan kwamba mapambano dhidi ya Taliban na washirika wao yataendelea hadi haki na uhuru utawale.