Jaji Onnoghen alisimamishwa kazi na Rais Mohammadu Buhari akimshutumu amevunja sheria inayomtaka mtendaji wa ngazi ya juu wa umma kujaza fomu akijielezea kiasi cha mali zake alipoteuliwa kama Jaji Mkuu wa taifa la Nigeria.
Baada ya kufungua mashtaka hayo Serikali ya Nigeria ilishindwa kutoa ushahidi dhidi ya Onnoghen na hivyo iliamua kufunga kesi hiyo.
Wakati huohuo upande wa utetezi uliomwakilisha Jaji umesema hauna tena sababu ya kuwaita mashahidi wake, lakini itaomba mahakama hiyo kutupia mbali kesi hiyo kwa sababu serikali ya Nigeria imeshindwa kuthibitisha madai yake.
Baadhi ya wananchi wa Nigeria wanadai kuwa hatua iliyochukuliwa na Rais Buhari, ni njama ya kumweka mwengine kutoka upande wa Kaskazini mwa Nigeria kuchukuwa cheo hicho cha Jaji Mkuu.
Madai yao pia yanalenga suala la njama ya kurudi tena madarakani wakidai kuwa Buhari alikuwa akijitayarisha kushindania urais awamu ya pili na iwapo angeshindwa kesi ikifikishwa Mahakama Kuu kabisa, atakuwa na mtu wake wa karibu atakaye mwonea huruma na kuhakikisha kwamba anapata ushindi.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Collins Atohengbe, Nigeria