Umoja wa Mataifa na Uturuki ulisimamia juhudi za usafirishaji nafaka kupitia Black Sea katikati ya mgogoro wa kimataifa wa chakula, ukitafuta njia ya kurahisisha usafirishaji huo uliokuwa umezuiwa na vita vya Russia nchini Ukraine.
Kabla ya makubaliano hayo kufikia muda wake wa mwisho Jumatatu, Russia ilisema kuwa haipati faida ya kutosha kutokana na juhudi hizi za usafirishaji.
Mkataba wa maelewano kati ya Moscow na Umoja wa Mataifa unataka kuondolewa vikwazo vya usafirishaji wa mbolea na nafaka za Russia.
Wakati chakula na mbolea havijawekewa vikwazo na nchi za Magharibi, juhudi zimefanyika kupunguza wasiwasi kwa mabenki, kampuni za bima, mashirika ya meli na watendaji wengine wa sekta binafsi wenye hofu ya kufanya biashara na Russia.
Moja ya madai makuu ya Russia yamekuwa yanahusu kurejeshwa kwa benki yake ya kilimo katika mfumo wa Swift wa malipo ya kifedha.
“Bahati mbaya, sehemu ya mikataba hii ya Black Sea inayohusiana na Russia haijatekelezwa hadi sasa, kwa hiyo utendaji wake umesitishwa,” msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amewaambia waandishi.
“Mara tu sehemu ya mikataba ya Russia itakapotekelezwa, upande wa Russia utarejea katika kutekeleza makubaliano hayo, mara moja.”
UN ilisema kuwa tangu usafirishaji nafaka ulipoanza Agosti 2023, tani za metrik 32.9 za chakula zilisafirishwa kwenda nchi 45. Wataalam walisema kutoendeleza makubaliano hayo kutasababisha bei ya chakula kupanda.
Meli ya mwisho kuondoka Ukraine chini ya makubaliano hayo ilianza safari kutoka bandari ya Ukraine Jumapili.
Baadhi ya taarifa katika habari hii zinatokana na mashirika ya habari ya AP, AFP na Reuters.