Ripoti ya Benki ya Dunia : Uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 5.2

Rais John Magufuli

Ripoti ya Benki ya Dunia iliyozinduliwa Alhamisi inaonyesha kuwa uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 5.2, mwaka 2018, kinyume na takwimu zilizokuwa zimetolewa na serikali ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters, Waziri wa Fedha wa Tanzania alikuwa ameliambia bunge mwezi Juni, 2019, uchumi wa nchi hiyo ulikua kwa asilimia 7, mwaka 2018.

Makadirio ya Benki ya Dunia yanaonyesha kwamba uchumi wa nchi hiyo utakua kwa asilimia 5.4 ikiwa ni chini ya asilimia 7.1 kwa mujibu wa makadirio ya serikali, Ripoti hiyo imeeleza.

Wakati wa uzinduzi wa Ripoti hiyo ya Benki ya Dunia Alhamisi iliyowasilishwa na Mchumi mwandamizi Bill Battaile wamesema wao hufanya hesabu zao kwa kutumia takwimu za Benki Kuu ya Tanzania na Mamlaka ya Kodi ya nchi hiyo.

Sababu zilizopelekea kuathiriwa kwa ongezeko hilo la uchumi wa mwaka 2018 kulitokana na kuanguka kwa viwango vya uwezekazji, mauzo ya soko la nje na mikopo sekta binfasi, ripoti hiyo imefafanua.

Rais John Pombe Magufuli alianzisha mpango wa kuimarisha sekta ya viwanda baada ya kuchukua hatamu mwaka 2015, akiwekeza mabilioni ya dola katika miundombinu, ikiwemo barabara ya reli, kufufua uchukuzi wa kitaifa wa angani pamoja na kiwanda cha umeme.

Lakini hatua ya serikali kuingilia sekta ya uchimbaji wa madini pamoja na ile ya kilimo imesababisha kupungua kwa uwekezaji katika sekta hizo katika taifa hilo linalotajwa kuwa la tatu kwa ukubwa kiuchumi Afrika mashariki, ilisema ripoti hiyo iliyochapishwa na Reuters.

Katika hotuba yake kuhusu hali ya uchumi wa taifa mwaka 2018 na mpango wa maendeleo wa mwaka wa fedha 2019/20 bungeni, Waziri wa Fedha na mipango Dkt Philip Mpango alisisitiza ukuuaji wa uchumi wa asilimia 7.0.

Naye Mchumi wa Benki ya dunia alisema : “Takwimu za NBS zinaonyesha pato la taifa (GDP) lilikua kwa asilimia 7.0, lakini Benki ya Dunia inaamini kasi hiyo ya ukuaji ilikuwa asilimia 5.2.

Kutokana na tofauti kati ya ripoti ya Benki ya Dunia na Wizara ya Fedha, Mkurugenzi mkuu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa, NBS, Dkt Albina Chuwa alihoji: “Sisi tuliopo ‘Field’ tunajua hali halisi. Takwimu zetu zinaoyesha uchumi umekua kwa asilimia 7.0 lakini ninyi mnasema ni asilimia 5.2. Kwa nini tofauti imekuwa kubwa kiasi hicho, vimeeleza vyanzo vya habari nchini humo.