Rais wa Ujerumani aomba msamaha kwa Watanzania kwa yaliyofanywa na utawala wa kikoloni

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier

Rais Frank-Walter Steinmeier siku ya Jumatano alielezea "aibu" yake kwa uhalifu uliofanywa wakati wa utawala wa kikoloni wa Ujerumani nchini Tanzania na kuahidi kuongeza ufahamu kuhusu uhallifu uliotendwa na nchi yake.

“Napenda kuomba msamaha kwa kile ambacho Wajerumani waliwafanyia mababu zenu hapa,” alisema Steinmeier alipotembelea Makumbusho ya Maji Maji, katika mji wa kusini wa Songea, kulingana na nakala ya hotuba yake

Tanzania ilikuwa sehemu ya German East Africa ambayo ilishuhudia uasi wa umwagaji damu zaidi katika historia ya ukoloni kati ya 1905 na 1907.

Wataalamu wanasema kati ya watu 200,000 na 300,000 wazawa wa eneo hilo waliuawa kikatili wakati wa kile kinachoitwa Uasi wa Maji Maji, hususani kutokana na uharibifu wa mashamba na vijiji uliofanywa na wanajeshi wa Kijerumani.

"Kilichotokea hapa ni historia yetu ya pamoja -- historia ya mababu zenu na historia ya mababu zetu huko Ujerumani," alisema, akiahidi "kuzichukua hadithi hizi pamoja nami hadi Ujerumani, ili watu wengi zaidi katika nchi yangu wazijue.

"Nataka kuwahakikishia kuwa sisi Wajerumani tutatafuta pamoja nanyi kupata majibu ya maswali ambayo hayajajibiwa ambayo hayawapi amani," aliongeza.

John Mbano, ambaye babu yake Chifu Songea Mbano aliuawa katika Uasi wa Maji Maji, alisema amefurahishwa maneno ya Steinmeier.

"Tumekuwa tukilia kwa miaka mingi, sasa ni wakati wa kumaliza kilio chetu," wakili huyo mwenye umri wa miaka 36 aliliambia shirika la habari la AFP kwa njia ya simu baada ya kukutana na rais wa Ujerumani mjini Songea.

Ziara hiyo ya kuyatembelea makumbusho ilikuja siku ya mwisho ya ziara ya siku tatu nchini Tanzania. Steinmeier, ambaye siku ya Jumanne pia alifungua milango ya kurejeshwa Tanzania kwa vitu vya kale vilivyoporwa wakati wa ukoloni.

Chanzo cha habari hii ni shiika la habari la AFP.