Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Novemba 22, 2024 Local time: 14:58

Ujerumani yaahidi kurudisha mafuvu ya binadamu yaliyochukuliwa Tanzania wakati wa ukoloni


Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier. Picha na REUTERS/Nadja Wohlleben/File Photo
Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier. Picha na REUTERS/Nadja Wohlleben/File Photo

Ujerumani iko tayari kwa mazungumzo na Tanzania kuhusu urithi wa miongo yake mitatu ya utawala wa kikoloni katika taifa la Afrika Mashariki, marais wa nchi hizo mbili walisema siku ya Jumanne.

Raisi wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier yuko katika ziara rasmi ya siku tatu nchini Tanzania.

Wanasiasa na wanaharakati wa Tanzania wamekuwa wakisisitiza kwa muda mrefu kuhusu fidia na kurejeshwa kwa mabaki ya binadamu yaliyochukuliwa kutoka nchini mwao ambayo yanaonyeshwa katika makumbusho nchini Ujerumani.

Rais wa Ujerumani Steinmeier alisema Ujerumani iko tayari kushirikiana na Tanzania katika "kurudisha mali za kitamaduni na mabaki ya binadamu".

"Hatupaswi kusahau yaliyopita," Steinmeier alisema baada ya kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan jijini Dar es Salaam katika siku ya pili ya ziara ya siku tatu nchini Tanzania.

Uhusiano kati ya nchi hizo mbili "umegubikwa na ukatili wa uvamizi wa ukoloni wa Kijerumani katika nchi hiyo ambayo ilijulikana kama German East Africa, " alisema Steinmeier.

“Tumelijadili hili kwa kina na tuko tayari kuanzisha mashauriano ili kuona jinsi tutakavyokubaliana kuhusu urithi wa ukoloni wa Kijerumani " Rais Samia Suluhu Hassan alisema katika mkutano na waandishi wa habari akiwa na rais mwenzake wa Ujerumani.

"Najua kuna familia ambazo zinasubiri mabaki ya ndugu zao walio katika makumbusho kadhaa nchini Ujerumani. Mazungumzo hayo yatatuongoza jinsi ya kulishughulikia suala hili vizuri,” alisema Samia.

Steinmeier, ambaye yuko katika ziara rasmi nchini Tanzania, alisema amepanga kukutana na watu walioathiriwa na uasi wa Maji Maji mwaka 1905 mpaka 1907 dhidi ya utawala wa kikoloni wa Ujerumani.

Watalaamu wanasema kati 200,000 na 300,000 idadi ya wazawa ambao waliuliwa kikatili wakati wa uasi huo wa Maji Maji wa mwaka 1905 mpaka 1907.

Ujerumani iliitawala Tanzania Bara, wakati huo ilipokuwa ikiitwa Tanganyika kuanzia miaka ya 1880 hadi 1918, ilipotekwa na vikosi vya Waingereza wakati wa Vita kuu ya Kwanza vya dunia.

Forum

XS
SM
MD
LG