Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Novemba 04, 2024 Local time: 21:07

Tanzania yatangaza mpango wa kuwandoa raia wake Israeli, yawataka kujiandikisha katika ubalozi mjini Tel Aviv


Waziri wa mambo ya Nje wa Tanzania January Makamba.
Waziri wa mambo ya Nje wa Tanzania January Makamba.

Serikali ya Tanzania imesema imeandaa mpango wa kuwarejesha nyumbani raia wake walio nchini Israeli wakati mzozo ukiendelea kati yake na wanamgambo wa Hamas.

Taaarifa iliyotolewa na wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania Jumamosi ilitoa wito kwa “Watanzania walio tayari kurejea nyumbani kujiandikisha kwenye Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliopo Tel Aviv.

“Kufuatia kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama nchini Israel na maeneo mengine jirani, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeandaa mpango wa kuwarejesha nchini Watanzania waliopo nchini humo na maeneo mengine ya karibu,” ilisema taarifa hiyo.

“ Serikali imefikia uamuzi huo baada ya kufanya tathmini na kujiridhisha kwamba mazingira ya sasa yanaruhusu zoezi hilo kufanyika. Hivyo, Watanzania walio tayari kurejea nyumbani wanashauriwa kujiandikisha kwenye Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliopo Tel Aviv, Israel kupitia barua pepe: telaviv@nje.go.tz au simu namba: +972 533 044 978 na +972 507 650 072, kabla ya tarehe 15 Oktoba 2023, saa 6 usiku,” iliongeza.

Mapema wiki hii, Balozi wa Tanzania nchini Israel Alex Kalua alisema hali inaendelea kuwa ya tahadhari huku watanzania wawili hawajulikani walipo na mwingine mmoja amepatikana baada ya shambulio la Hamas nchini Israel mwishoni mwa juma.

Kuna jumla ya watanzania wapatao 260 nchini humo ambao wengi wao ni wanafunzi.

Kwa mujibu wa balozi huyo serikali ya Israel imewataka wasikae kwa wasi wasi na wanaendelea kupata taarifa kutoka kwao kila jioni na wameeleza kuwa ikiwa kuna kundi lolote litahitaji kuondoka nchini humo linaweza kwani viwanja vya ndege vyote vinafanya kazi kama kawaida.

Baadhi ya maeneo ya Tel Aviv na Kusini mwa Israel kulikuwa na taharuki lakini mamlaka za nchi hiyo zinatoa taarifa kwa umma na kila nyumba ina eneo salama la kujificha (Shelter) na iwapo ikitokea tahadhari watu wanaweza kukimbulia maeneo hayo salama.

Mamlaka imewatahadharisha wananchi kutotoka nje na wakae karibu na nyumba zao ili ikitokea hatari wapate fursa ya kukimbilia kwenye eneo salama kwa urahisi.

Forum

XS
SM
MD
LG