Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 22, 2024 Local time: 20:47

Shinikizo la kumtaka Mfalme Charles kuomba radhi na kulipa fidia laongezeka Kenya


Rais wa Kenya William Ruto na Mfalme Charles wa Uingereza walipowasili kwenye Kaburi la Shujaa Asiyejulikana jijini Nairobi Oktoba 31, 2023. Picha na Victoria Jones / POOL / AFP.
Rais wa Kenya William Ruto na Mfalme Charles wa Uingereza walipowasili kwenye Kaburi la Shujaa Asiyejulikana jijini Nairobi Oktoba 31, 2023. Picha na Victoria Jones / POOL / AFP.

Mfalme wa Uingereza Charles III na mkewe Malkia Camilla wamewasili nchini Kenya usiku wa kuamkia Jumanne kwa ziara ya siku nne, na kukutana na rais wa Kenya William Ruto katika ikulu ya Nairobi.

Wakati huo huo, shinikizo likiongezeka la kutaka fidia na kuomba radhi kutokana na madhara pamoja na dhuluma zilizofanywa na utawala wa kikoloni wa Uingereza nchini humo wakati wa uasi wa Mau Mau.

Akiiwakilisha serikali ya Uingereza, Mfalme Charles, ziara hii itaimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili wenye misingi ya ushirikiano wenye nguvu.

Kulingana na Ikulu, rais Ruto na mgeni wake, wamejadiliana kuhusu masuala kadhaa yanayolenga kuimarisha ustawi wa pande zote mbili.

Wakati ujumbe wa mawaziri ulioongozwa na mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi na waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza James Cleverly wamekutana na kujadiliana kuhusu nafasi za ushirikiano hususani katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, kukuza fursa na ajira kwa vijana, kuendeleza maendeleo endelevu pamoja na kuunda eneo thabiti na salama, na vile vile nyanja za sanaa ya ubunifu, teknolojia, elimu na uvumbuzi pamoja na biashara.

Ingawa ziara hii inalenga misingi hiyo ya kuboresha mahusiano kati ya Uingereza na Kenya, na pia uwepo wa mwitikio wa mfalme Charles wa kutambua machungu ya historia kati ya Uingereza na Kenya kati ya mwaka 1952 hadi 1960 na nia yake ya kutaka kufahamu madhara yaliyofanywa katika kipindi hicho cha kihistoria.

Gitu Wa Kahengeri, Katibu Mkuu wa Chama cha Mashujaa wa Vita vya Mau Mau wakati wa mahojiano na shirika la habari la AFP Oktoba 13, 2023. Picha na SIMON MAINA / AFP.
Gitu Wa Kahengeri, Katibu Mkuu wa Chama cha Mashujaa wa Vita vya Mau Mau wakati wa mahojiano na shirika la habari la AFP Oktoba 13, 2023. Picha na SIMON MAINA / AFP.

Baadhi ya Wakenya wakiwemo wanaharakati, wapigania uhuru wameitaka serikali ya Uingereza kuwalipa fidia waliopitia manyanyaso ya kikoloni na pia kumtaka Mfalme Charles kuiomba radhi Kenya kutokana na madhara waliyoyapata mashujaa wa uhuru.

Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya, shirika lisilo la kiserikali, imesema Mfalme Charles anapaswa kuomba msamaha kwa unyanyasaji uliofanywa na Uingereza wakati wa ukoloni.

Wawakilishi wa jamii za Wamaasai nchini Kenya na Tanzania vile vile, wanamtaka Mfalme kutambua dhuluma za kihistoria ambazo wamedai zilipelekea kunyang’anywa mashamba yao na walowezi na kuwaingiza katika matatizo ya kijamii na kiuchumi na hivyo wanataka Mfalme Charles kupendekeza mpango wa kuwarejeshea ardhi yao pamoja na fidia.

Wanaharakati wa haki za binaadamu na wapigania uhuru wa zamani wakiwa wameshikilia mabango na kuimba nyimbo za kupinga ziara ya Mfalme Charles III wa Uingereza nchini Kenya Picha na LUIS TATO / AFP.
Wanaharakati wa haki za binaadamu na wapigania uhuru wa zamani wakiwa wameshikilia mabango na kuimba nyimbo za kupinga ziara ya Mfalme Charles III wa Uingereza nchini Kenya Picha na LUIS TATO / AFP.

Hata hivyo, maandamano na mikusanyiko ya aina yote imedhibitiwa wakati wa ziara hii.

Baadhi ya jamii za Kenya, zikiwemo za Kikuyu, Nandi, Pokot na Kipsigis pia zimemtaka Mfalme Charles kuomba msamaha na fidia ya kifedha kutokana na dhuluma za kihistoria zilizofanywa na serikali ya Uingereza wakati wa utawala wa kikoloni.

Jamii hizi pia zimeitaka serikali ya Uingereza kurejesha mali za kitamaduni wanazodai zilinyakuliwa na utawala wa kikoloni wakati ambapo Kenya inaadhimisha miaka 60 ya uhuru wake.

Mfalme Charles, mkewe Malkia Camila pamoja na rais Ruto na ujumbe wake, Jumanne mchana wamezuru Bustani ya Uhuru ambayo sasa ni Mnara wa Kitaifa na Makumbusho ya mashujaa waliopigania uhuru wa Kenya, uliopo dakika 15 kutoka katikati mwa jiji la Nairobi, ambako waasi dhidi wakoloni Waingereza walisherehekea siku ya Uhuru mwaka 1963 na hadhi ya jamhuri mwaka 1964.

Sasa ni uwanja wa kutafakari juu ya mapambano ya nchi ya uhuru na mafanikio ya baada ya Uhuru wa Kenya.

Mfalme Charles wakati wa hafla ya kuweka shada la maua kwenye Kaburi la Shujaa Asiyejulikana huko Nairobi Oktoba 31, 2023. Picha na Victoria Jones / POOL / AFP.
Mfalme Charles wakati wa hafla ya kuweka shada la maua kwenye Kaburi la Shujaa Asiyejulikana huko Nairobi Oktoba 31, 2023. Picha na Victoria Jones / POOL / AFP.

Mfalme Charles na Mkewe Camila wameweka shada la maua ikiwa ni ishara ya kutoa heshima kwa eneo ambalo uhuru wa Kenya ulitangazwa mwaka 1963.

Miaka miwili iliyopita, Kenya na Uingereza zilitia saini mkataba wa kiuchumi kwenye lengo la kuimarisha biashara na uwekezaji kati ya nchi hizi mbili na pia kutangaza maafikiano mapya ya mkataba wa ulinzi ambao unasisitiza ushirikiano wa juhudi za kukabiliana na ugaidi na kuruhusu wanajeshi wa Uingereza kupata mafunzo nchini Kenya.

Baadaye, Mfalme Charles na mkewe Malkia Camila wanatarajiwa kuzuru Pwani ya Kenya kwenye Kituo cha Wanamaji cha Mtongwe mjini Mombasa na kuwatazama wanajeshi wanamaji wa Kenya, waliofundishwa na wanajeshi wa Uingereza, na ushirikiano wa ulinzi uliopo kati ya vikosi hivyo.

Mfalme Charles ameshawahi kufanya ziara rasmi nchini Kenya mara tatu mwaka 1971, 1978 na 1987. Lakini hii ndio ziara ya kwanza tangu kutawazwa kuwa Mfalme wa Uingereza.

TAARIFA HII IMEANDARIWA NA KENNEDY WANDERA, SAUTI YA AMERIKA, NAIROBI.

Forum

XS
SM
MD
LG