Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 18:50

Tanzania yatia saini mkataba na DP World kuhusu bandari ya Dar es Saalam


Mwenyekiti wa DP World Sultan bin Sulayem wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya kibiashara ya Dibai Expo 2020.
Mwenyekiti wa DP World Sultan bin Sulayem wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya kibiashara ya Dibai Expo 2020.

Tanzania Jumapili imetia saini mkataba na kampuni inayomilikiwa na serikali ya Dubai ya DP World, ya kuendesha shughuli kwenye bandari ya Dar es Saalam kwa miaka 30 ijayo, hatua ambayo imekuwa ikipingwa vikali na upinzani pamoja na makundi ya kutetea haki.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Plasduce Mbossa ambaye ni mkurugenzi mkuu wa Halimashauri ya Bandari ya Tanzania TPA, inayoendesha shughuli kwenye bandari hiyo amesema kwamba DP World itakodisha na kuendesha gati 12 za bandari hiyo, ambayo ni kubwa zaidi nchini Tanzania.

Bandari hiyo pia huhudumia mataifa jirani yasiyo na bandari kama vile Uganda, Rwanda, Burundi na Zambia yenye utajiri mkubwa wa shaba. Mbossa ameongeza kusema kwamba mkataba huo ni wa miaka 30, na kwamba utakuwa ukichukuliwa tathmini kila baada ya miaka 5.

Ametetea hatua hiyo akisema kwamba itaimarisha utendakazi wa bandari hiyo kwa kupunguza muda wa kuondoa makontena, pamoja na kuhudumia meli 130 kwa mwezi, kulinganishwa na 90 kama ilivyo kwa sasa.

Mwenyekiti na mkurugenzi mkuu wa DP World Sultan Ahmed Bin Sulayem wakati wa kusaini mkataba huo mjini Dodoma amesema kwamba kampuni yake itawekeza dola milioni 250 ndani ya miaka 5 ijayo, katika kukarabati bandari hiyo, ili kuimarisha uwezo wake.

Forum

XS
SM
MD
LG