Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 05, 2024 Local time: 19:27

Wanasheria Tanzania wanataka mikataba ya DP World kuwekwa wazi


Waziri wa Uchukuzi Makame Mbarawa akiwa na Mwenyekiti mtendaji wa DP world, Sultan Ahmed bin Sulayem mara baada ya kusaini mkataba.
Waziri wa Uchukuzi Makame Mbarawa akiwa na Mwenyekiti mtendaji wa DP world, Sultan Ahmed bin Sulayem mara baada ya kusaini mkataba.

Wanasheria nchini Tanzania wameitaka serikali kuweka wazi mikataba mitatu ya uwekezaji na uendeshaji wa bandari kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na DP World ili kuhakikisha maoni ya wananchi yamesikilizwa na kufanyiwa kazi.

Wakati uwekezaji huo unatarajiwa kuongeza ufanisi katika uendeshaji na utoaji huduma pamoja na kuongeza ajira kwa Watanzania.

Wanasheria na wachumi waliiambia Sauti ya Amerika wana mashaka na mikataba hiyo wakidai kuwa, baadhi ya vipengele vilivyofichika vitaweza kuleta athari baadaye. Hivyo wanaitaka serikali kuiweka mikataba hiyo wazi ili kuwaruhusu wananchi kuthibitisha kama maoni yao yamesikilizwa na kufanyiwa kazi inavyostahili.

Wakili Boniface Mwabukusi amesema, serikali inapaswa kuiweka wazi mikataba iliyosainiwa ili iweze kujadiliwa kitaalamu na kutoa fursa kwa wananchi kufahamu kile walichokuwa wakikilalamikia katika mkataba wa utangulizi wa IGA kama umefanyiwa marekebisho yaliyohitajika.

“mkataba wauweke wazi ili tuweze kutoa maoni kitaalamu kwasababu kwa sasa hatuelewi kinachoendelea tunajaribu kukisikia tu. Na hata mkataba wa utangulizi wa IGA haujabadilishwa mpaka sasa” alisema Mwabukusi.

Uwekezaji huo unatarajiwa kuongeza makusanyo ya kodi, ushuru wa forodha, na tozo mbalimbali ambapo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatarajiwa kukusanya shilingi za Tanzania trillion 26.7 ifikapo mwaka 2032.

Baadhi ya viongozi na wageni waliohudhuria hafla ya utiaji saini uwekezaji na uendeshaji wa sehemu ya bandari huko Chamwino, tarehe 22 Oktoba.
Baadhi ya viongozi na wageni waliohudhuria hafla ya utiaji saini uwekezaji na uendeshaji wa sehemu ya bandari huko Chamwino, tarehe 22 Oktoba.

Naye Martin Cheger, mhadhiri mwandamizi kutoka shule ya uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema matarajio ya Watanzania wengi ni kuona ufanisi katika uendeshaji wa bandari unaongezeka pamoja na ajira ili kusaidia kukuza uchumi wa taifa na Watanzania kwa ujumla.

“Tunategemea ufanisi uongezeke katika uendeshaji na utoaji huduma katika bandari yetu lakini vilevile uzalishaji na ajira vinaongezeka. Hayo ni mambo ambayo tunategemea yakifanyika basi uchumi wa Tanzania utaongezeka, alisema.

Mwakilishi kutoka Jukwaa la Sauti ya Watanzania Dkt. Wilbroad Peter Slaa aliiambia Sauti ya Amerika kuwa hawakubaliani na mikataba hiyo iliyosainiwa na wataendelea na maandamano yasiyo na kikomo ili kushinikiza kufutwa kwa mikataba hiyo.

“Sisi tutaendelea na taratibu zetu ambazo tulikwisha kupanga ikiwa ni pamoja na maandamano yasiyokoma kushinikiza wananchi kukataa mikataba hiyo kwasababu hakuna serikali inayofanya kazi bila kufuata taratibu za kawaida ikiwa pamoja na taratibu za kupata vibali vya bunge” alisema Slaa.

Hata hivyo wakati wa utiaji saini mikataba hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan alisisitiza kwamba mkataba huo utawanufaisha wananchi na kuchangia katika maendeleo ya nchi huku akitoa ahadi kwamba hakuna Mtanzania atakayepoteza ajira yake bandarini.

Imetayarishwa na Amri Ramadhani, Sauti ya Amerika, Dar es Salaam

Forum

XS
SM
MD
LG