Msaidizi huyo alikuwa amesafiri nje ya nchi akiwa ameambatana na Membe na wote wawili walirejea nchini humo mwanzoni mwa wiki hii.
Polisi inasema msaidizi huyo anayetambulika kwa jina la Jerome Luanda alikamatwa muda mfupi wakati alipowasili nchini humo akitokea Dubai.
Kamanda wa Kanda maalumu ya Dar es salaam, Lazaro Mambosasa ametupilia mbali taarifa kwamba alikamatwa na watu wasiojulikana na katika mazingira ya kutatanisha.
Amesema alikamatwa mchana kweupe na maafisa wa jeshi hilo wakati akiwa na bosi wake, Membe.
Mambosasa amesema sababu za kutiwa mbaroni kwa msaidizi huyo zinahusiana na tuhuma za utakatishaji wa fedha na kwamba jeshi hilo linaendelea kumhoji na iwapo litajiridhisha litamfikisha mahakamani.
Kamanda huyo hakueleza zaidi sababu za kukamatwa kwa afisa huyo wa Membe kama kuna uhusiano wowote na safari yake ya nje ya nchi aliyoifanya wiki iliyopita au la.
Membe amekuwa akishutumu hatua hiyo na kusisitiza kwamba yuko tayari kwenda mbali zaidi kuhakikisha msaidizi huyo anaachiwa huru.
Kukamatwa kwa msaidizi huyo kunafanyika wakati mgombea huyo wa ACT Wazalendo akisitisha kwa muda kampeni zake na hivi karibuni alifunga safari hadi Dubai alikodai alikwenda kwa ajili ya kuhudhuria mkutano ulioandaliwa na kampuni moja ambayo naye ni miongoni mwa wakuregenzi wake.
Baadhi ya wakosoaji wake walidai kwamba safari hiyo waliyoiita ya ghafla ilikuwa na malengo ya kisiasa wakihisi pengine alikuwa amekwenda kusaka ushawishi ikiwemo wa kifedha. Hata hivyo, Memba alikanusha vikali madai hayo.
Membe anajikuta katika hali hiyo wakati wagombea wenzake wa urais wakiendelea kuchanja mbuga kukutana na wapiga kura katika mikutano ya kampeni.
Wagombea wote wametawanyika mikoani ambako sasa wanajiandaa kumaliza wiki ya tatu tangu walipopuliza rasmi kipenga cha kuanza kampeni mwishoni mwa mwezi wa Agosti.