Papa awahimiza mahasimu wa kisiasa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa Sudan Kusini

Papa Francis akihudhuria mkutano baada ya mkutano wa faragha wa kiroho wa siku mbili ambao ulihudhuriwa na viongozi wa Sudan Kusini leaders at the Vatican, April 11, 2019.

Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki, Papa Francis, katika kitendo cha kihistoria ambacho hakijawahi kushuhudiwa, Alhamisi alipiga magoti na kuibusu miguu ya viongozi wa Sudan Kusini, ambao awali walikuwa mahasimu wa kisiasa, na kuwasihi wasirejee kamwe katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Ujumbe wa kiroho wa Papa

Papa aliwahimiza viongozi hao kuahidi kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa ifikapo mwezi Mei.

"Macho ya Mungu yanawaangalia. Na ni macho ambayo yanawaletea amani. Lakini pia kuna jicho jingine, jicho la raia wa nchi yenu, ambao wanataka kuona haki, maridhiano na amani," alisema Papa.

Katika ziara hiyo Makanisa yamewakilishwa na wanachama wanane wa baraza la Makanisa la Sudan Kusini.

Mkutano wa faragha

Papa Francis alifanya hivyo baada ya kumaliza mkutano wa faragha na viongozi hao, huko Vatican, katika juhudi za kuleta amani nchini kwao.

Wakati wa mkutano wao, Papa Francis aidha aliwataka Rais Salva Kiir, aliyekuwa Makamu wa Rais wa kwanza ambaye aligeuka na kuwa muasi, Riek Machar, na makamu wengine watatu wa rais, kuheshimu makubaliano ya kudumisha amani, na kuheshimu makubaliano ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa mwezi Mei.

Kiir na Machar walianza mkutano huo na Papa Francis siku ya Jumatano, kwa madhumuni ya kutafuta njia ya kuleta amani ya kudumu katika taifa hilo changa zaidi duniani.

Papa awakutanisha mahasimu wa kisiasa

Mahasimu hao wakubwa walikutakana katika jumba la Casa Santa Marta , ndani ya Vatican, ambalo ni kasri la kale la kuwapokea wageni, na makazi yake Papa Francis, ambaye alichagua makazi hayo alipochaguliwa mwaka 2013, badala ya makao rasmi ambayo kiutamaduni, viongozi wengine wa Kanisa Katoliki walikokuwa wakiishi.

Kasri hiyo isiyovutia ndipo mahala yalipofanyika mazungumzo ya kihistoria ya amani kati ya aliyekuwa Rais wa Israeli, Shimon Peres na Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas mwaka 2014.

Kuhusu mkutano wa wiki hii, Papa Francis alisema mazungumzo yao yalikuwa ni kutoa fursa ya wote kwa pamoja kusimama mbele ya Mungu na kusikiliza matakwa yake.

Ujumbe wa Papa

Papa amesema katika ujumbe wake: "Ni nafasi ya kutathmini maisha yetu na mipango ambayo Mungu anayo kwetu. Ni kutambua wajibu mkubwa wa pamoja kwa sasa na kwa mustakabali wa watu wa Sudan Kusini, na kujitolea, tukiwa na nguvu na urafiki, ili kulijenga taifa lenu.

Kiir na Machar walikuwa wameonana kwa mara ya mwisho mwezi Oktoba 2019, muda mfupi baada ya kuweka saini makubaliano ya amani, wakati Machar alipotembea mjini Juba, kwa muda mfupi, kwa mara ya kwanza tangu kuondoka kufuatia mapigano ya 2016.

Kiir akutana na Waziri Mkuu wa Italia

Wakati huohuo Kiir alikutana na Waziri Mkuu wa Italia, Giuseppe Conte mapema Jumatano kabla ya kuelekea Vatican, ambako alitarajiwa kukutana na maafisa wa serikali ya mseto, inayotarajiwa kuundwa mwezi Mei.

Katika mkataba huo, Machar atarejeshewa kushikilia mamlaka yake ya makamu wa rais.

Makamu wengine waliohudhuria mkutano huo ni James Wani Igga, Taban Deng Gain a Rebecca Nyandeng De Mabior.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, CD