Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 20:28

Odinga anapendekeza awe msuluhishi wa Sudan Kusini


Kiongozi mkuu wa upinzani Kenya, Raila Odinga
Kiongozi mkuu wa upinzani Kenya, Raila Odinga

Kiongozi wa upinzani nchini kenya na aliyewahi kuwa Waziri Mkuu nchini humo, Raila Odinga alisema anadhani anaweza kuleta tofauti katika mazungumzo yaliyokwama kati ya Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir na kiongozi wa waasi Riek Machar.

Odinga alipendekeza kuwa mpatanishi wa mazungumzo hayo katika lengo la kukomesha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanaoendelea kwa karibu miaka mine na nusu sasa. Kiongozi huyo mkuu wa upinzani Kenya alitembelea Juba kwa ziara ya faragha wiki mbili zilizopita na kukutana na Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, siku kadhaa baada ya vyama hasimu kushindwa kufikia mkataba wa amani katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.

Waziri wa habari wa Sudan Kusini, Michael Makuei alisema kuwa wakati wa ziara hiyo, Odinga alieleza kwamba aliwataka Kiir na Machar kufikia muafaka kama ambavyo yeye na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya walivyofanya baada ya tofauti zao zilizokuwepo siku za nyuma.

Riek Machar (L) na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini
Riek Machar (L) na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini

Gazeti la East African liliripoti kwamba Odinga anatarajia kusafiri kwenda Afrika kusini wiki hii kukutana na Machar. Msemaji wa waasi alisema Machar anashikiliwa katika kifungo cha nyumbani na maafisa wa Afrika kusini kufuatia ombi la utawala wa Kiir. Hata hivyo maafisa wa Kiir wanakanusha madai hayo.

Makuei alisema anatarajia Odinga ataweza kufahamu vyema masuala yenye utata kati ya pande zinazogombana kabla ya kukutana na Machar. Pia anatarajia Odinga kumshawishi Machar kusitisha ghasia.

Aidha, waziri Makuei aliiambia VOA kwamba “jambo la kwanza na muhimu ni kulaani uhasama. Odinga anahitaji kufahamu ni mipango gani waliyonayo wengine. Ndani ya mapendekezo haya ambayo yamewasilishwa, baadhi yao hayawezekani kamwe kutekelezwa, na hawawezi kwa njia yeyote ile kufikia kiwango cha kupatikana amani. Hivyo basi anatakiwa kufanya kazi kulainisha msimamo wa upinzani.”

Michael Makuei, waziri wa habari Sudan Kusini
Michael Makuei, waziri wa habari Sudan Kusini

Makuei alifafanua misimamo ya Machar isiyokubalika ikiwa ni pamoja na kuvunja vyombo vyote vya usalama nchini humo na kuikabidhi Ofisi ya Umoja wa Mataifa huko Sudan Kusini- UNMISS.

Makuei alisema utawala wa Kiir unatarajia juhudi za Odinga kusaidia mazungumzo ya amani yanayoongozwa na jumuiya ya ushirikiano wa serikali za pembe ya Afrika na Afrika mashariki-IGAD ambayo yalimalizika bila makubaliano kufikiwa mwezi uliopita huko Ethiopia. Pande zinazohasimiana hazikukubaliana juu ya mfumo wa kushirikiana madaraka au mpango kamili wa kuwaingiza wapiganaji wa makundi ya waasi katika jeshi la Sudan Kusini.

XS
SM
MD
LG