Papa alikumbusha Kanisa Katoliki kuwa waumini wanasubiri haki itendeke

Viongozi wa Kanisa Katoliki wanaohudhuria mkutano wa kihistoria, Vatican, Alhamisi Feb 21, 2019.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis anaongoza mkutano wa kihistoria, Vatican, Alhamisi, unaojadili jinsi ya kukabiliana na manyanyaso ya ngono dhidi ya watoto yaliyodumu kwa miongo kadhaa.

Katika siku ya kwanza ya mkutano huo wa siku nne Francis amewaambia viongozi wa Kanisa Katoliki kwamba Waumini wao “wanaangalia na kusubiri” viongozi hao wachukue “hatua madhubuti na zenye kujitosheleza” kukabiliana na unyanyasaji wa kingono na sio tu kulaani vitendo hivyo vya manyanyaso ya ngono kiholela vilivyofanywa na wachungaji hao.

Kashfa ya manyanyaso ya ngono yanayo wahusisha viongozi wa Kanisa Katoliki, limeleta mtikisiko mkubwa katika kanisa hilo kote duniani.

Papa amesisitiza kuwa waliohudhuria mkutano huo “wasikilize kilio cha waumini ambao wanataka haki itendeke.”

Mkutano huo unakusudia kuwaelimisha viongozi wa kanisa namna ya kukabiliana na tuhuma za manyanyaso ya ngono na kuwafariji waathirika, pamoja na kuzuia vitendo kama hivyo kutokea siku za usoni.

Kashfa hiyo imeligubika Kanisa dunia nzima kwa miongo mitatu, na kuwepo ripoti mbalimbali zinazoeleza kuwa maafisa wa ngazi ya juu wa kanisa walikuwa wakiwalinda viongozi waliokuwa wakituhumiwa kuwaharibu watoto.

Papa Francis yeye mwenyewe anakosolewa kwa kushindwa kusimamia ipasavyo kesi ya manyanyaso ya ngono iliyowahusisha viongozi wa dini huko Chile mwaka 2018, kwa madai kuwa kanisa lilificha matendo yao hayo.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC