Mwandishi wa habari za uchunguzi auawa Ghana

Taasisi ya Tiger Eye inashughulika na habari za uchunguzi

Mwandishi wa habari za uchunguzi Ghana ameuawa kwa bunduki wakati akiwa ndani ya gari lake akielekea nyumbani.

Vyanzo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa watu wasio julikana wakitumia usafiri wa pikipiki walimpiga risasi tatu Ahmed Hussein-Suale mjini Accra.

Suale alipigwa risasi mbili kifuani na moja shingoni majira ya usiku Jumatano, vyanzo hivyo vimeeleza.

Marehemu alikuwa ni mdau wa taasisi binafsi ya Tiger Eye na alikuwa akichunguza vitendo vya rushwa katika ligi ya mpira wa miguu Ghana.

Baada ya kuibua kashfa hiyo ya rushwa kiongozi wa shirikisho la kandanda nchini Ghana alifungiwa kutoshiriki katika shughuli za kandanda maisha.

Baada ya taarifa za kashfa hiyo kutangazwa na chombo cha kimataifa mbunge wa Ghana Kennedy Agyapong alisambaza picha za mwandishi huyo Hussein-Suale na kutaka adhabu dhidi yake.

Shirika la habari la BBC limeripoti kuwa mwandishi huyo wa habari za upelelezi aliwahi kushirikiana nao katika taarifa kadhaa ikiwemo upelelezi wa uuzaji wa viungo vya watu kwa ajili ya shughuli za kichawi huko Malawi.