Jack Dorsey aliwatangazia wafuasi wake milioni 4 Jumamosi kwamba alikuwa amezuru Myanmar kaskazini mwezi Novemba kwa siku kumi za kutafakari kwenye eneo lenye utulivu, na kuwashawishi watembelee nchi hiyo.
"Watu wanafuraha tele na chakula ni cha kipekee," aliwashauri wafuasi wake kutembelea huko.
Lakini hilo limeibua lawama kutoka kwa baadhi watu wakisema amepuuza hatma ya walio wachache katika jamii ya Kiislam ya Rohingya wanaoishi Myanmar.
Jeshi la Myanmar, mwaka 2017, liliripotiwa kuanzisha operesheni ya kuwasaka wanamgambo wa Rohingya baada ya vituo kadhaa vya polisi kushambuliwa.
Maelfu ya watu wameuawa na taasisi zinazopigania haki za binadamu zinasema jeshi lilichoma nyumba na ardhi na kuendesha mauaji na ubakaji.
Wakati majeshi ya Myanmar yakifanya mashambulizi hayo dhidi ya wanamgambo wa Rohingya, yanayo daiwa na vikundi vya haki za binadamu kupitiliza mipaka, na watu zaidi ya 700,000 wa jamii ya Rohingya walikimbilia nchi jirani ya Bangladesh kutafuta hifadhi, baada ya makazi yao na ardhi zoa kuharibiwa kwa kuchomwa moto.
Umoja wa Mataifa umetaja kitendo hicho cha jeshi la Myanmar kuwa ni mfano wa kuiangamiza jamii na kusema kuwa maafisa wa vyeo vya juu nchini Myanmar wanastahili kuchunguzwa kwa makosa ya jinai ya uhalifu wa kivita.