Umoja wa Mataifa unasema kuwa idadi mpya ya wakimbizi wanaowasili hapo inaongezeka kutokana na msukumo unaotokana na vitendo vya uvunjifu wa amani katika nchi jirani ya Myanmar tangu mwisho wa Agosti kufikia watu 536,000 kama ilivyoripotiwa na VOA.
Ripoti iliyotolewa Jumatano huko Geneva na ofisi ya haki za binadamu ya UN imewatuhumu wanajeshi wa Myanmar, wakisaidiwa na makundi ya wanajeshi wakibudha wenye silaha, kwamba siyo tu wameshambulia majumba ya Waislam wa Rohingya na vijiji vyao lakini pia wamekuwa wakijaribu “kuondoa kabisa alama na kumbukumbu zote za watu hao katika ardhi yao” huko eneo la Rohingya ili kufanya watu hao wasiweze kuwepo kabisa katika nchi hiyo.
Zaidi ya wakimbizi nusu milioni wamekimbia Myanmar kuelekea eneo la Bangladesh Cox Bazar tangu Agosti 25, wakati mashambulizi katika vituo vya usalama yalipofanywa na wapiganajiwa Rohingya na kusababisha majeshi ya Myanmar kutumia nguvu kupita kiasi kupambana nao.
Lakini ripoti ya UN iliyokuwa imejikita katika mahojiano 65 iliyofanya na mamia ya wakimbizi, imesema kuwa operesheni ya kuwaondosha Waislam wa Rohingya huko eneo la Rakhine ilianza mapema kwa mwezi moja takriban.
Wakimbizi wamewaambia wachunguzi wa UN kwamba hata kabla ya mashambulizi na baada yake, vyombo vya usalama vilitumia vipaza sauti kuwashinikiza Waislam kukimbia eneo hilo na kutafuta hifadhi huko Bangladesh, la sivyo “tutachoma nyumba zenu na kuwaua.”
Pia Waislam wa Rohingya wameeleza visa vilivyofanywa na vyombo vya usalama ikiwemo kuwapiga risasi wanavijiji na ubakaji wa makundi kwa wasichana wadogo chini ya miaka mitano yaliofanywa na askari wasio na magwanda.
Wimbi kubwa la wakimbizi wa Rohingya takriban 11,000 tayari wamewasili kupitia mpakani mwa nchi hiyo wakiingia Bangladesh Jumatatu. Msemaji wa UN katika masuala ya wakimbizi Andrej Mahecic amesema kuwa ilivyokuwa eneo la mpakani liko shuwari, lakini ameongeza kuwa bado watu wanahangaika nchini Myanmar wakijaribu kuondoka kuelekea Bangladesh.
"Bila shaka kuna idadi kubwa ya watu wameripotiwa au wanasubiri kuvuka mto Naf kwa kutumia maboti na kisha kuvuka Bangladesh.”
Operesheni kubwa ya misaada inaendelea kufanyika huko eneo la Cox Bazar, Bangladesh, ambapo mashirika ya misaada yamekuwa yakiwasaidia wakimbizi hao sehemu za kuishi, chakula, maji, usafi na mahitaji mengine muhimu. Shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu na Shirika la Mwezi Mwekundu lina wasiwasi juu ya upatikanaji wa mahitaji mbalimbali muhimu ya afya katika jamii hizo za wakimbizi.
Mkurugenzi wa Afya wa Red Cross Julie Hall amesema kliniki zinazotumia magari tayari zimeweza kuwasaidia zaidi ya watu 4,000, lakini huduma hizo bado hazitoshelezi kabisa. Amesema kuwa shirika lake liko mbioni kutayarisha hospitali ya rufaa yenye vitanda 60.
“Hili litafanyika kati ya kambi mbili kubwa. Itaweza itapoanza kutoa huduma, kuwa na kitengo cha upasuaji, ukunga na wagonjwa wa nje pamoja na maabara, etc. Na hii itakuwa ni huduma inayotolewa siyo tu kwa wahamiaji lakini pia kwa wenyeji wa eneo hilo waliowapokea wakimbizi hao.
Mbali na hatua hizi, mashirika hayo yanafanya juhudi kupunguza na kuzuia maambukizi. Kampeni ya chanjo ya cholera inaendelea kwa masiku kadhaa. WHO imeripoti kuwa watu 235,000 kati ya walengwa 650,000 kati ya walengwa wa kampeni hiyo tayari wamepewa chanjo hiyo dhidi ya maradhi hayo hatarishi.