Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 22:17

Marekani : Jeshi la Myanmar linahusika na mauaji ya Warohingya


Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana- kujadili kadhia ya Myanmar mwaka mmoja baada ya kuanza mgogoro wa wakimbizi.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana- kujadili kadhia ya Myanmar mwaka mmoja baada ya kuanza mgogoro wa wakimbizi.

Mwaka mmoja baada ya Waislam walio wachache wa kabila la Rohingya kukimbia kwa makundi kutoka Myanmar, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imekusanya ushahidi kutoka kwa wale walio nusurika na mauaji unaothibitisha tuhuma kuwa jeshi la Myanmar na vikosi vya usalama vilitekeleza uvunjaji wa kinyama wa haki za binadamu.

“Ushahidi wa moja kwa moja ulio tolewa na wale walio nusurika unaonyesha kuwa wengi wa wananchi wa Rohingya walikabiliwa moja kwa moja na uvunjifu wa amani, ima katika nyumba zao, familia zao au yote mawili,” Balozi wa Marekani Nikki Haley ameuambia mkutano wa Baraza la Usalama juu ya kadhia hiyo.

“Jambo muhimu kuliko yote, ambalo ripoti inaliainisha ni kikundi kimoja ambacho kina husika na utekelezaji wa sehemu kubwa ya vitendo hivi vya uhalifu huu – jeshi la Burma na vikosi vya usalama,” amesema, akitumia jina jingine la nchi hiyo ya Myanmar.

Uchunguzi wa Wizara ya Mambo ya Nje

Haley amesema yaliyo gunduliwa na Wizara ya Mambo ya Nje yanatokana na zaidi ya mahojiano 1,000 yaliyo fanywa kwa kuchagua baadhi ya wakimbizi katika kambi iliyoko Bangladesh. Takriban Warohingya 700,000 walikimbilia huko baada ya mashambulizi ya kinyama ya jeshi la Burma baada ya wanamgambo wa Rohingya kushambulia na kuuwa dazeni ya vikosi vya usalama vya Myanmar.

Yaliyo orodheshwa katika ripoti

Haley aliorodhesha kutoka katika ripoti hiyo ambayo bado haijatolewa kwa umma. Kati ya yaliogunduliwa ni:

* Moja ya tano ya watu wote wa kabila la Rohingya walio hojiwa wamesema walishuhudia zaidi ya wahanga 100 wakiuwawa au kujeruhiwa;

*Asilimia 82 ya wakimbizi walishuhudia nyumba zao au kijiji chao kikiangamizwa;

*Asilimia 51 imesema walishuhudia unyanyasaji wa kingono;

*Asilimia 65 walishuhudia mmoja wa mwanafamilia au mwanakijiji mwenzao akijeruhiwa.

“Watoto wadogo, wachanga, wanawake na wanaume waliathiriwa na uhalifu wa kinyama,” Haley amesema. Mashambulizi hayo yalikuwa yamepangwa, yamekusudiwa na kuratibiwa. Walio endesha uhalifu huo walikuwa ni jeshi la Burma na vikosi vya usalama.”

Mambo waliofanya viongozi wa kijeshi

Mapema mwezi huu, uongozi wa Trump uliiwekea vikwazo vilivyowalenga makamanda wa watano wa jeshi la Myanmar na vikundi viwili vya jeshi kwa kuhusika na mauaji hayo.

Yaliyogunduliwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani yanaakisi matokeo ya uchunguzi wa kujitegemea uliofanyika na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa. Jopo hilo lilitoa ripoti hiyo siku ya Jumatatu.

Ripoti ya Jopo la UN

Jopo hilo katika majumuisho yake lilieleza kuwa hatua ya jeshi la Myanmar katika kujibu mashambulizi ya wanamgambo wa Rohingya ulikuwa wa “haraka, kikatili na haulingani na shambulizi dhidi yao kwa ujumla.” Jopo hilo limesema kuna uwezekano mkubwa kuwa shambulizi hili lilipangwa mapema.

Imewataja maafisa sita ya jeshi la Myanmar, akiwemo Mkuu wa Majeshi Jenerali wa ngazi ya juu Min Aung Hlaing, ikisisitiza kuwepo kwa uchunguzi na kufunguliwa mashtaka juu ya uhalifu dhidi ya binadamu, ikiwemo mauaji ya halaiki.

XS
SM
MD
LG