Shambulizi la Msikitini New Zealand : Serikali yawahakikishia Waislam miili itakabidhiwa haraka, yatoa sababu za umuhimu wa uchunguzi

Familia, jamaa na marafiki wa Naeem Rashid aliyeuawa na mtoto wake Talha Naeem msikitini Christchurch, New Zealand, wakifanya maombi maalum katika makazi ya wahanga hao, katika mji wa Abbottabad, Pakistan, Macih 17, 2019.

Kamishna wa Polisi nchini New Zealand Mike Bush amesema Jumapili kuwa mwili mmoja wa muhanga wa mauaji yaliyofanyika katika misikiti ya Ijumaa mjini Christchurch utaanza kukabidhiwa kwa familia ya marehemu kuanzia Jumapili usiku.

Naye Mkuu wa uchunguzi wa mauaji nchini humo Deborah Marshall amesema ofisi yake “inashughulikia kwa haraka iwezekanavyo” kuhakikisha inakabidhi mwili sahihi wa familia husika. “Hakuna kitu kibaya zaidi,” amesema, kuliko kutoa mwili wa marehemu kuwapa familia isiyohusika.

Vyanzo vya habari vimeripoti kuwa taarifa iliyotolewa na kusambazwa kwa familia za wahanga hao, watu waliokufa ni kati ya umri wa miaka 3-77. Baadhi ya wahanga walitokea maeneo jirani, na wengine walitokea mbali kama vile Misri ama Fiji. Takriban watu wawili miongoni mwa waliokufa- mtoto na baba- walitokea familia moja.

Ufafanuzi juu ya uchunguzi wa miili ya wahanga

Makamu wa Kamishna Wally Haumaha amesema Jumapili kuwa ofisi yake imeshakutana na viongozi wa jumuiya ya Kiislam kusaidia kuwafahamisha juu ya umuhimu wa mchakato wa vipimo vya miili hiyo kuchukuwa muda mrefu kwa ajili ya uchunguzi wa jinai iliyofanyika dhidi yao. Amesema kuwa wanafahamu kuwa katika utamaduni wa Kiislam maiti hutakiwa kuzikwa ndani ya saa ishirini na nne.

Serikali inamatumaini itakuwa imekabidhi miili yote ya wahanga wa tukio hilo kwa familia zao ifikapo Jumatano. Orodha ya awali ya wahanga imetolewa kwa familia zao, polisi wamesema.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Ujerumani imesema mkuu mmoja wa shule Sheikh Amjad Ali alinukuliwa akisikitika kuwa, "tayari wameuawa, nini kingine wanataka kujua?", hii ikiwa ni kutokana na kucheleweshwa kutolewa kwa miili hiyo.

Sababu za uchunguzi huo

Deborah alisisitiza kuwa "miili ya waliofariki ilitakiwa pamoja na mambo mengine kufanyiwa vipimo vya mionzi, kuchukuliwa alama za vidole, mpangilio wa meno na kufanyiwa uchunguzi wa kina.

Mume asema hana kinyongo na muuaji

Farid Ahmad mwenye miaka 44 ambaye mkewe Husna aliuawa wakati alipokuwa akikimbilia kutoka msikitini kujiokoa, alikataa kumlaumu mshambuliaji na badala yake alisema "ningalipenda kumwambia kwamba nampenda kama alivyo". Alisema hayo alipozungumza na shirika la habari la AFP.

Kulingana na vyombo vya usalama, watu 34 bado wamelazwa hospitalini. Miongoni mwao ni mtoto wa miaka minne Alin Alsati, aliyekuwa akiswali na baba yake Waseeim katika msikiti wa Al Noor, ambaye alipigwa risasi mara tatu.

Tamko la Tarrant lilimfikia Waziri Mkuu

Waziri Mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern amesema Jumapili kuwa yeye ni kati ya zaidi ya watu 30 waliotumiwa tamko la itikadi ya kibaguzi iliyotumwa kupitia barua pepe na mshukiwa wa muuaji ya watu 50, Brenton Tarrant, dakika tisa kabla ya shambulizi lake la mrengo wa kulia la kigaidi katika misikiti miwili New Zealand. Tamko hilo lilikuwa linawalaani Waislam na pia kuwaita wahamiaji ni “wavamizi”.

Amesema kuwa tamko hilo lilitumwa katika ofisi yake na “yeye hakulipokea moja kwa moja” na wala halikuelezea sehemu ambayo shambulizi hilo la mauaji litafanyika.

Ardern amesema Tarrant, miaka 28, Raia wa Australia na mwenye msimamo binafsi wa itikadi za kibaguzi amefunguliwa mashtaka ya mauaji kuhusiana na tukio la kuwapiga bunduki watu misikitini “ bila shaka sheria itachukuwa mkondo wake kwa kumhukumu kwa vitendo vyake nchini New Zealand.

Mabadiliko ya sheria ya kumiliki silaha

Hapo awali baada ya tukio Ardern aliyaita mauaji hayo ya umma “kitendo cha uvunjifu wa amani kisichokuwa cha kawaida.” Alisema kuwa mshambuliaji huyo aliyetumia bunduki alikuwa na bunduki tano, mbili kati ya hizo ni zenye uwezo wa kurusha risasi nyingi kwa wakati mmoja. Silaha zote hizo zilikuwa zimenunuliwa kwa kufuata sheria.

Waziri Mkuu huyo ametoa tamko mara kadhaa wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari Jumapili kuwa “Lazima kutafanyika mabadiliko ya sheria zetu za kumiliki silaha.”