Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, kaimu afisa mkuu wa mamlaka hiyo, Dan Elwell, alisema Jumanne kwamba uchunguzi uliofanywa kufikia sasa, haujabaini hitlafu yoyote na mfumo wa Ndege hizo na kwa hivyo haoni haja ya kusitisha safari zake.
Ajali hiyo ilipelekea nchi kadhaa kutangaza kusitishwa kwa safari za Ndege, za muundo kama huo, zikiwa ni pamoja na China, Uingereza na Ethiopia.
Mashirika matatu ya Ndege nchini Marekani, Southwest Airlines, American Airlines na United Airlines yamesema Ndege hizo za 737 Max zitaendelea na safari, hata ingawa baadhi ya abiria waliandika jumbe mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii, wakilelezea hofu yao na kuuliza kama ndege hizo zinaweza kubadilishwa.
Haya yalijiri katika siku ambayo mamlaka ya usafiri wa angani ya Umoja wa ulaya ilitangaza marufuku ya ndege hizo katika anga za nchi wanachama wa muungano huo.
Mapema Jumanne, maombolezi yaliendelea huku risala za rambirambi zikiendelea kutolewa kwa jamaa za watu 157 waliopoteza maisha yao wakati ndege hiyo ya shirika la ndege la Ethiopia ilipoanguka karibu na Addis Ababa siku ya Jumapili.
Waathirika hao ni kutoka nchi tofauti 35 ikiwa ni pamoja na wafanyakazi 22 wa Umoja wa mataifa waliokuwa wakielekea Nairobi kwa mkutano mkuu wa mazingira, UNEA.
Bendera kwenye ofisi za Umoja huo zilipepea nusu mlingoti.